KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushushwa kwenye fainali za kuwania taji la Tim Wanyonyi Super Cup 2021 kitengo cha wanaume na wanawake zitakaopigiwa ugani Kihumbu-ini Kangemi, Nairobi.
Kwa wanaume mabingwa watetezi, Leads United ya kocha, Wilston Issa itaingia mzigoni kukabili Wazoefu FC kwenye patashika inayotazamiwa kuwa ya kukata na shoka. Nao warembo wa Patriots Queens watashika dimbani kukutanishwa na City Park.
”Bila shaka tunafahamu bayana kuwa mchezo huo hautakuwa mteremko. Wapinzani wetu wamejipanga kutubomoa na kubeba taji la mwaka huu,” kocha wa Leads alisema na kuongeza katika mashindano yoyote huwa wanalenga kushiriki fainali.
Kwenye nusu fainali ya mechi hizo , Leads United iliangusha wenzao wa Young Boys kwa mabao 5-4 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare tasa. Nayo Wazoefu FC ilichapa City Park B FC mabao 3-2 kwenye patashika iliyoshuhudia ushindani wa kufa mtu.
Wafungaji wa Wazoefu FC walikuwa Nelson Mandela, Gerrison Gikono na Francis Kairu waliotikisa wavu mara moja kila mmoja. Nao Peter Ng’ang’a na Dismas Machak kila mmoja alifungia City Park B. Kwenye mechi za kina dada, Kangemi Ladies ya kocha, Loice Karanja ilijikuta kwenye wakati mgumu ilipozimwa kuzoa tiketi ya kushiriki fainali.
NAPITA: Wachezaji wa Leads United wakicheza na Young boys kwenye nusu fainali ya kuwania taji la Tim Wanyonyi Super Cup 2021 ugani Kihumbu-ini Kangemi, Nairobi. Leads ilishinda mabao 5-4 kupitia mipigo ya matatu baada ya kutoka sare tasa… Picha/JOHN KIMWERE
Vipusa hao walitandikwa kwa magoli 5-4 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. Nayo Patriots Queens ilifanya kweli ilipocharaza Real Starlets kwa mabao 2-1 na kunasa tiketi ya fainali.
Katika robo fainali za wanaume, Leads United ilizaba ,Kipande FC bao 1-0, Young Boys ilicharaza Brookside mabai 2-1, PAG Kangemi ilinyukwa bao 1-0 na Wazoefu FC nayo City Park B ilisajili ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Kitusuru Allstars.
Kwa kina dada, Patriots Queens ilizaba Rhunda View kwa mabao 6-0. Real Starlets ilipata ushindi wa mezani baada ya Gachie Friends kuingia mitini. Vipusa wa Kabete Chicks walifungwa mabao 2-0 na City Park Ladies huku Kangemi Ladies ikikung’uta Kabete Ladies kwa mabao 2-0. Kinyang’anyiro cha mwaka huu kilivutia timu 65 za wanaume na 14 za wanawake.
NAPITA: Wachezaji wa Leads United wakicheza na Young boys kwenye nusu fainali ya kuwania taji la Tim Wanyonyi Super Cup 2021 ugani Kihumbu-ini Kangemi, Nairobi. Leads ilishinda mabao 5-4 kupitia mipigo ya matatu baada ya kutoka sare tasa…Picha/JOHN KIMWERE