GWIJI WA WIKI: DJ Kezz
NA CHRIS ADUNGO
NDOTO ya kuwa mwanamuziki ilianza kumtambalia Keziah Jerono Rachel katika umri mdogo.
Mamaye mzazi alimruhusu ajiunge na makundi mbalimbali ya uimbaji kanisani na shule pia ikampa fursa nyingi za kushiriki mashindano ya ngazi na viwango tofauti.
Akiwa mwanafunzi wa darasa la nne, alikuwa tayari amekwea ngazi ya muziki wa injili kiasi cha kuwa sehemu ya kwaya ya Kanisa la Kiadventista la Kapsowar iliyofyatua albamu yenye nyimbo nane za Kiswahili, ‘Ujumbe’, mnamo 2004.
Kipawa cha ulumbi pia kilimfanya kuwa maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake na akawa tegemeo la makundi yaliyoburudisha wazazi na kutumbuiza wageni nyakati za mikutano muhimu shuleni.
Aliwahi kuongoza shule ya upili ya Torongo Girls iliyoko Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo, kufika kiwango cha kitaifa kwenye tamasha za muziki zilizofanyika jijini Nairobi 2011 na 2012.
Mnamo 2018, Keziah alisomea uDJ katika Chuo cha Swag Sound mjini Eldoret. Alijikuza zaidi katika fani hiyo akiwa na kikundi cha Hits Republic kilichompa majukwaa tele ya kutononoa kipaji chake kuanzia 2019 akitumia lakabu ‘DJ Kezz Kenya’.
Janga la corona lililoingia humu nchini mnamo 2020 lilizima ghafla ziara zake za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya burudani na akaanza safari ya wokovu.
Alioanisha maarifa ya uDJ na ujuzi wa kiteknolojia na kuanzisha kipindi cha mitandaoni cha ‘Adventist Sabbath’ alichokitumia kueneza Ukristo na kucheza nyimbo za wasanii mbalimbali wa Kiadventista.
Keziah alijitosa kikamilifu katika ulingo wa muziki mnamo Mei 2020 kwa kujiunga na kundi maarufu la Msanii Music lililoanzishwa na waimbaji Waadventista wa Sabato pekee kabla ya kufungulia milango waumini wa madhehebu mengine.
Japo angali katika kundi hilo, alianza kutoa nyimbo zake binafsi mnamo 2021. ‘Kimbilio’ ni kibao alichokiachilia Novemba mwaka huo, miezi mitatu kabla ya Msanii Records kumchomolea ‘Naendea Msalaba’.
Alianza kushirikiana kimuziki na msanii Guardian Angel mnamo Aprili 2022 na wakaachilia nyimbo tatu – ‘Jipende’, ‘Unaweza’ na ‘Hapa Kwetu’ – chini ya mwavuli wa Seven Heaven Music.
Mwanzoni mwa Novemba 2022, Keziah alishirikiana na nyanya yake, Bi Rachel Yano, kutoa albamu ndogo ya nyimbo nne (EP). Mbali na kibao ‘Lango’ alichokicharaza kwa pamoja na Angel, albamu hiyo, ‘Abaibai’, ina nyimbo tatu ambazo amezisana kwa Kikalenjin – ‘Abaibai’, ‘Kaagas’ na ‘Atinye Chorwet’.
Kubwa zaidi katika maazimio yake kisanaa ni kuchomoa kibao kipya kila baada ya mwezi mmoja. Anapania pia kupanua wigo wake wa ukulima na ujasiriamali.
Keziah alilelewa katika eneo la Kapsowar, Kaunti ya Elgeyo Marakwet. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watatu wa Bi Elly Jerop.
Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kapsowar (2000-2005) kabla ya kujiunga na Chemweno Tophill Academy, Elgeyo Marakwet (2006-2008) kisha shule ya upili ya Torongo Girls (2009-2012).
Ana shahada ya masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Moi (2013-2018).
Next article
Raila kupewa mamlaka iwapo Mswada utapita