Connect with us

General News

Eunice Kemunto – Taifa Leo

Published

on

Eunice Kemunto – Taifa Leo


GWIJI WA WIKI: Eunice Kemunto

KISWAHILI ni miongoni mwa lugha kuu za Kiafrika zinazozungumzwa na idadi kubwa zaidi ya watu duniani.

Sensa ya Canada ya 2006 iliripoti wazungumzaji 27,795 wa Kiswahili nchini humo na idadi hiyo ilitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 22 kufikia mwisho wa mwaka jana.

Eunice Kemunto Marube ni miongoni mwa Wakenya ambao ni mabalozi wa Kiswahili nchini Canada. Ingawa ni mhasibu kitaaluma, yeye ni mwimbaji stadi wa nyimbo za injili.

Alilelewa katika mtaa wa Pangani jijini Nairobi na ndiye mwanambee katika familia ya watoto watano wa Bw Henry Marube na Bi Jane Kerubo.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Juja Road, Nairobi (1986-1994) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Pangani Girls (1995-1998). Alisomea shahada ya B.Com (Accounting) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (2000-2003).

Mnamo Agosti 2004, Eunice alitumwa na Kanisa la Kiadventista la Kariokor hadi Canada kuwa sehemu ya washiriki wa kongamano lililopania kuwapa vijana malezi ya kimaadili na kuwafundisha ujuzi wa kuchangia maendeleo ya jamii kwa uzalendo, umoja na ukakamavu.

Alisalia huko na akaajiriwa kuwa mhudumu katika kituo kimoja cha mafuta kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kurejelea kazi yake ya uhasibu mnamo 2007. Eunice kwa sasa ni mhasibu katika Serikali ya Mkoa wa Saskatchewan.

Ingawa kipaji cha uimbaji kilianza kujikuza ndani yake utotoni, ilikuwa hadi 2017 alipojitosa rasmi katika ulingo wa muziki wa injili na akazindua albamu yake ya kwanza mnamo Julai mwaka huo.

Albamu hiyo, ‘Pendo Lake’, ina nyimbo nne ambazo amezisana kwa Kiswahili – ‘Pendo Lake’, ‘Yanipasa’, ‘U Wangu’ na ‘Uliniumba’.

‘Mipango Yako’ ni albamu ya pili ya nyimbo 10 aliyoichomoa 2018; mwaka mmoja kabla ya kufyatua vibao 10 alivyovihifadhi katika albamu ‘Worship With Hymns’.

Tangu atoe albamu ‘Yahweh’ ya nyimbo 13 mnamo 2020, Eunice alicharaza vibao sita mnamo 2021 na kuachilia nyimbo tatu zaidi mwaka wa 2022.

Mwimbaji wa nyimbo za injili, Eunice Kemunto Marube ambaye kwa sasa ni mhasibu nchini Canada. PICHA | CHRIS ADUNGO

Kibao chake cha hivi karibuni zaidi ni ‘Nalindwa na Yesu’ alichokitoa Januari 27, 2023. Amerekodi nyimbo nane tayari akiwa na mpango wa kuchomoa mmoja mmoja kila baada ya miezi miwili.

Katika albamu ya ‘Yahweh’, alishirikisha wasanii Christina Shusho, Upendo Nkone, Solomon Mkubwa na Rose Muhando ambaye ameimba naye nyimbo mbili – ‘Tambarare’ na ‘Yahweh’.

Zaidi ya kutumia muziki kueneza Ukristo na kupigia Kiswahili chapuo, kubwa zaidi katika maazimio ya Eunice ni kusaidia wasiojiweza katika jamii, kuwa mlezi wa vipaji miongoni mwa vijana na kupiga vita ndoa za mapema na dhuluma dhidi ya wanawake kupitia mpango wa Divine Voice Foundation aliouanzisha mwaka wa 2020.

Mama huyu wa watoto watatu pia ni mwandishi wa vitabu vya ushauri nasaha. Aliandika ‘Broken But Blessed’ mnamo 2018; miaka miwili kabla ya kuchapisha ‘Surviving Loss: How to Navigate Pain’.

Anashikilia kuwa siri ya kufaulu katika ulingo wa muziki ni kumtanguliza Mungu, kujiamini na kujituma.

“Usijitose ulingoni kwa ajili ya fedha au umaarufu. Utafadhaika sana. Ingia iwapo una kiu ya kutumia kipaji chako kubadilisha maisha ya wanajamii kwa njia chanya,” anashauri.Source link

Comments

comments

Facebook

Trending