Connect with us

General News

Hadhari iwepo katika kubuni maneno ya lugha ya Kiswahili – Taifa Leo

Published

on


NGUVU ZA HOJA: Hadhari iwepo katika kubuni maneno ya lugha ya Kiswahili

NA PROF CLARA MOMANYI

HAKUNA lugha isiyotanuka na kukua duniani.

Kila lugha hukua kulingana na mabadiliko katika jamii, yawe ni ya kiteknolojia, kidini au hata kiutamaduni. Aidha, lugha huweza kunyauka hata kufa kama vile tanzu za mti zinavyonyauka na kukauka.

Katika lugha, hali hii hutokea pale ambapo hakuna wazungumzaji wa kuikuza na kuidumisha kama vile mti unapokosa huduma ya maji au hata virutubishi, hukauka hadi mizizini.

Lugha ikiwa na wazungumzaji hai, bila shaka itakuwa katika hali ya kusambaa, kutanuka na kudumu kwa muda mrefu hasa pale inapoandikiwa vitabu na kuhifadhiwa kwa njia mbalimbali.

Kiswahili kina historia ndefu andishi hususan ya kifasihi, kuliko lugha nyingine yoyote ya kiasili nchini Kenya. Kasi ya maendeleo ya lugha hii ni jambo la kufurahisha hasa kwa wenyeji wa Afrika Mashariki.

Hata hivyo, hatuna budi kuchukua tahadhari pale tunaposhabikia ubunifu wa maneno unaotokana na mabadiliko mbalimbali katika jamii.

Maneno hubuniwa yakatumiwa, lakini wapo wazungumzaji wataona vigumu kutumia au hata kutamka baadhi ya maneno hayo, kwa kawaida huyapiga pande wakayasahau kabisa. Mfano ni pale ambapo neno linakuwa gumu kutamkika, au linaudhi baadhi ya watu hasa linapotumiwa katika miktadha fulani.

Katika kubuni maneno au hata istilahi, tusisahau kwamba Kiswahili kina nyenzo zake zinazotumiwa katika uundaji wa maneno na ukubalifu wa maneno hayo na wanajamii. Ijapokuwa hatuna chombo cha kutathmini na kupima ufaafu wa baadhi ya maneno yanayoundwa hii leo, tunahitaji kutochukulia kimzaha au kiholela uundaji huo.

Kuna baadhi ya maneno yanayoundwa hii leo ambayo hayazingatii kanuni za lugha hii katika uundaji. Maneno yaliyomo pia huweza hata kuborongwa yakachukua sura mpya kabisa, yakatumiwa hadi kuchukuliwa kuwa sahihi. Hapa pia tusiulaumu msimbo wa Sheng ati ndio unaoharibu Kiswahili bali tuangalie ufaafu wa maneno tunayounda kila kukicha, mengine yakitumiwa hata na wanafunzi darasani kimakosa. Mifano ya maneno hayo ni mingi. Tufahamu kwamba lugha ni chombo kinachostahili kutunzwa na kuheshimiwa ili kiifae jamii inayokitumia.

Prof. Clara Momanyi, Ph.D., EBS.