MWALIMU WA WIKI: Kirika atamba si darasani si ugani
Na CHRIS ADUNGO
MWALIMU bora ni rafiki wa wanafunzi wote anaowafundisha.
Kutokana na ukaribu wao, wanafunzi huwa radhi kabisa kumweleza matatizo yao bila uoga wowote.
Mwalimu aliye na mlahaka mwema na wanafunzi wake hutambua kwa urahisi udhaifu wa kila mmoja wao na hivyo kujiweka katika nafasi murua zaidi ya kuwasaidia na kuwaelekeza ipasavyo.
Zaidi ya kuwasilisha somo darasani, mwalimu pia ni mzazi wa wanafunzi wote, mlezi wa vipaji vyao na mshauri wao kuhusu masuala mbalimbali maishani.
Haya ni kwa mujibu wa Bw John Ndirangu Kirika ambaye sasa ni mwalimu wa Kiswahili na somo la Dini katika shule ya Kagondo iliyoko Kaunti ya Nyandarua.
“Mwalimu bora anastahili kuwa kielelezo chema na awahimize wanafunzi kwamba wana uwezo wa kufaulu masomoni. Awe karibu nao, aelewe kiwango cha mahitaji ya kila mmoja wao, awaelekeze kimaadili na awaamshie hamu ya kuthamini masomo,” anaelezea.
Kwa mtazamo wa Bw Kirika, mwalimu bora ni mwajibikaji, mbunifu na mwepesi wa kuchochea wanafunzi wake kupiga hatua kubwa katika safari ya elimu inayohitaji subira.
Kirika almaarufu Kirika wa Warufaga, alilelewa katika kijiji cha Matuiku, eneo la Elburgon, Kaunti ya Nakuru. Ndiye wa nne kuzaliwa katika familia ya watoto watano wa Bi Mary Njeri na marehemu Bw Philip Ndirangu.
Alianza safari ya elimu katika chekechea ya Reli iliyoko Elburgon mnamo 1995 kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya Michinda, Elburgon (1996-2003) kisha shule ya upili ya Elburgon (2004-2007).
Ingawa alitamani kuwa daktari, alisomea ualimu (Kiswahili/Dini) katika Chuo Kikuu cha Chuka (2008-2011). Aliyemchochea kujitosa katika ulingo wa ufundishaji ni Bw Gachoka aliyempokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya upili. Bw Gachoka kwa sasa ni Mwalimu Mkuu katika shule ya upili ya Njenga Karume Molo, Nakuru.
Kabla ya kuhitimu, Kirika alishiriki mafunzo ya nyanjani katika shule ya Mpukoni iliyoko Chuka, Kaunti ya Tharaka Nithi na akapata kibarua cha kufundisha katika shule ya Mtwapa Elite Mombasa (2012-2014).
Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri 2015 na kumtuma kufundisha katika shule ya Manyatta iliyoko Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua. Alihamia Kagondo mnamo 2020.
Uzoefu anaojivunia katika ufundishaji na utahini wa Kiswahili umemwezesha kuzuru shule nyingi za humu nchini kwa nia ya kuhamasisha walimu na kuelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.
Mbali na ualimu, Kirika amekuwa pia akiwashirikisha wanafunzi wake kwenye mashindano ya ngazi na viwango tofauti katika mchezo wa soka uliomfungulia fursa ya kuwa kocha tangu mwaka wa 2011.
Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwa mwakilishi na mtetezi wa maslahi ya walimu kupitia vyama vya walimu nchini Kenya kabla ya kujiendeleza kitaaluma na kuwa mhadhiri wa Kiswahili katika vyuo vikuu.
Kwa pamoja na mkewe Bi Bilha Ndung’u, wamejaliwa watoto wawili – Trevis Ndirangu na Kendrah Njeri.