Connect with us

General News

Seneta Omtatah kuelekea kortini kupinga mpango wa ubinafsishaji wa mashirika ya serikali bila idhini ya Bunge – Taifa Leo

Published

on

Seneta Omtatah kuelekea kortini kupinga mpango wa ubinafsishaji wa mashirika ya serikali bila idhini ya Bunge – Taifa Leo


Seneta Omtatah kuelekea kortini kupinga mpango wa ubinafsishaji wa mashirika ya serikali bila idhini ya Bunge

NA CHARLES WASONGA

SENETA wa Busia Okiya Omtatah ameapa kuwasilisha kesi mahakamani kupinga mpango wa Rais William Ruto wa kuuza mashirika ya serikali bila idhini ya Bunge.

Bw Omtatah alisema ataelekea kortini wiki ijayo kuzuia kujadiliwa kwa Mswada wa Ubinafsishaji, 2023 “kwa sababu bunge limetekwa na Ikulu ya Rais”.

“Sharti Wakenya wasimame na kutekeleza mamlaka yao kulingana na kipengele cha 1 (1) na (2) cha Katiba na wapinge pendekezo hili. Hii ndiyo maana kwa niaba yao, nitaelekea kortini wiki ijayo kupinga mswada huu,” akawaambia wanahabari katika Majengo ya Bunge, Jumatano.

Mnamo Jumanne, Baraza la Mawaziri liliidhinisha Mswada wa Ubinafsishaji, 2023 unaopendekeza kuuzwa kwa mashirika ya serikali bila idhini ya Bunge.

Mswada huo unampa Waziri wa Fedha mamlaka kubinafisha mashirika hayo kwa msingi kuwa utaratibu wa zamani wa kusaka idhini kutoka bungeni ulizongwa na “urasimu mwingi.”

Pendekezo hilo pia limepingwa na wabunge wa mrengo wa Azimio ambao wameapa kupinga mswada huo utakapowasilishwa bungeni.

Bw Omtatah alisema mswada huo unakwenda kinyume na Katiba kwa sababu unalipokonya Bunge wajibu wake wa kuhakiki utendakazi wa Serikali Kuu.

“Mswada huu unapaswa kuwasilishwa kwa wananchi ili wauidhinishe katika kura ya maamuzi,”, akaeleza.

Kulingana na seneta huyo kipengele cha 255 (1) (h) cha Katiba kinasema kuwa mswada wowote ambao unaufanyia marekebisho majukumu ya bunge sharti uidhinishwe katika kura ya maamuzi.

“Hili pendekezo la kutwa mali ya Serikali na kuiweka mikononi mwa watu wenye ushawishi kwa kisingizio cha kubinafsisha ni baya na hatutakubali litekelezwe katika enzi hii ambapo Kenya inaongozwa na Katiba inayotilia maanani uwazi na uwajibikaji,” Bw Omtatah akasema.

Seneta huyo wa Busia alisema ikiwa serikali imeshindwa kusimamia mashirika ya serikali, suluhu liko katika kushughulikia matatizo hayo na sio kuyauzwa kwa sekta ya kibinafsi.

Lakini kulingana na Baraza la Mawaziri, kuuzwa kwa mashirika ya umma yasiyo na umuhimu wakati huu au yanayoandikisha hasara, kutasaidia katika kuimarishwa kwa miundo msingi na utoaji huduma kwa Wakenya.

Endapo mswada huo utapitishwa bunge, itakuwa umebatilisha ya sasa kuhusu ubinafishaji iliyopitishwa mnamo 2005. Sheria hiyo inamhitaji Waziri wa Fedha kuwasilisha ripoti kuhusu pendekezo la ubinafishaji kutoka kwa baraza la mawaziri hadi kwa kamati husika ya Bunge ili ijadiliwe na kupitisha au kukataliwa.

Mswada wa sasa unapendekeza kubuniwa kwa Mamlaka ya Ubinafsishaji na unampa Waziri wa Fedha mamlaka ya kuteua mwanachama wa mamlaka hiyo.

Wakosoaji wa mswada wanasema wajibu  huu ambao Waziri wa Fedha amepewa yataingilia uhuru wa  Mamlaka hiyo ya Ubinafsishaji.



Source link

Comments

comments

Facebook

Trending