Connect with us

General News

Shambulio jingine Lamu laharibu mashine za ujenzi – Taifa Leo

Published

on


Shambulio jingine Lamu laharibu mashine za ujenzi

Na KALUME KAZUNGU

WAVAMIZI wanaoshukiwa kuwa magaidi Jumapili walivamia kambi ya ujenzi wa barabara eneo la Kwa Omollo, karibu na Bodhei, msituni Boni, Kaunti ya Lamu na kuchoma matingatinga, malori na vifaa vingine vya ujenzi.

Uvamizi huo ulitekelezwa majira ya saa kumi usiku.

Inadaiwa walijigawa makundi matatu kabla ya kuvamia kambi hiyo inayolindwa na wanajeshi wa KDF.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alithibitisha shambulio hilo akasema maafisa wa usalama tayari wameanzisha msako wa waliohusika.

“Walinda usalama wetu walikabiliana nao vilivyo na kuwashinda. Hakuna aliyeuawa wala kujeruhiwa kwenye makabiliano hayo,” akasema.

Shambulio la jana la linajiri wiki moja baada ya kaunti ya Lamu kushuhudia mashambulio yaliyowaacha watu 15, ikiwemo maafisa wanne wa polisi wakiuawa na nyumba zaidi ya kumi zikichomwa kwenye vijiji vya Widho, Juhudi-Ukumi, Mashogoni, Marafa na Bobo-Sunkia.