Connect with us

General News

Ubabe kati ya Matiang’i, Ongwae wachacha wakiunga Raila – Taifa Leo

Published

on


Ubabe kati ya Matiang’i, Ongwae wachacha wakiunga Raila

Na WYCLIFFE NYABERI

MVUTANO umeibuka baina ya wafuasi wa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i na Gavana wa Kisii, Bw James Ongwae kuhusu ni nani anayefaa kuongoza kampeni za kumpigia debe kinara wa ODM Raila Odinga katika eneo la Gusii.

Hii ni baada ya Bw Ongwae kuteuliwa mmoja wa maafisa watakaoendesha kampeni za Bw Odinga, huku wadhifa atakaotekeleza Dkt Matiang’i katika jaribio la tano la Bw Odinga kuingia Ikulu ya Nairobi ukiwa haujabainika.

Licha ya viongozi hao kutoonyesha hadharani kuwa wamegawanyika, duru zinasema kuna vita baridi vinavyoendelea kuhusu anayefaa kuongoza kampeni za Bw Odinga eneo la Gusii ambalo huwa halipigi kura kwenye kapu moja.

Katika hafla za Gavana Ongwae, baadhi ya madiwani wamekuwa wakimhimiza aiongoze jamii ndani ya Azimio la Umoja huku Dkt Matiang’i anapozuru kaunti za Nyamira na Kisii, baadhi ya wanasiasa humsawiri kama anayefaa kuiongoza jamii katika meza ya kugawa rasilmali za kitaifa.

Wengi wanaomuunga mkono Bw Ongwae kuwa msemaji wa jamii ya Abagusii katika siasa za kitaifa ni madiwani, Mwakilishi wa kike Bi Janet Ong’era na Seneta wa Kisii Profesa Sam Ongeri.

Lakini kwa upande wake, Dkt Matiangi amewavuta baadhi ya wabunge wanaoheshimika katika jamii hiyo.

Wao ni mbunge wa Kitutu Chache Kusini Bw Richard Onyonka, Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Bw Simba Arati, mwenzake wa Nakuru mjini Magharibi Samuel Arama, Mwakilishi wa kike kaunti ya Nyamira Bi Jerusha Momanyi na hata seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni.

Jumapili iliyopita katika eneobunge la Bomachoge Chache, wakati wa kumzika mamake naibu gavana wa Kisii, siasa za Bw Ongwae kuiongoza jamii ya Abagusii zilirindimwa na baadhi ya viongozi waliosema kuwa yeye ndiye amekuwa mshirika wa karibu wa Bw Odinga kwa muda mrefu.

Viongozi hao walisema Gavana Ongwae amekuwa akizunguka Kenya yote na Bw Odinga na hivyo anafaa kumpigia debe eneo hilo.

Wakosoaji wa Dkt Matiang’i waliokuwepo walisema yeye amekuja hivi maajuzi katika kambi ya Bw Odinga na ni kufuatia maridhiano ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga maarufu kama Handisheki mwaka 2018.

“Tunajua Gavana Ongwae amehudumu kwa mihula miwili na miaka hiyo kumi inatosha kuiongoza jamii yetu kisiasa,” akasema Bi Ong’era kwenye mazishi ya Tendere.

Semi kama hizo zilitolewa na anayetafuta kiti cha ugavana wa Kisii kupitia chama cha Kenya National Congress, Bw Manson Oyongo.

Alipoongoza hafla za kuchangisha pesa kufadhili ujenzi wa shule mbali mbali katika kaunti ya Nyamira mwezi Desemba 2021, viongozi wanaounga Dkt Matiang’i nao walisema ni yeye anayefaa kuiongoza jamii yao na hayo yamekuwa yakirudiwa kwenye hafla anazoongoza.

“Wakisii wacha niwaeleze, mtoto wetu hapa nyumbani Dkt Fred Matiang’i, ametosha na tunafaa kumuunga mkono na ni yeye anayefaa kutuongoza,” akasema mwakilishi wa kike Bi Jerusha Momanyi katika shule ya upili ya Rioga, ambako Dkt Matiang’i alikuwa na hafla za kufadhili ujenzi wa bweni la kisasa.Source link

Comments

comments

Facebook

Trending