Connect with us

General News

Upweke wajaa Ford Kenya Olago naye aking’oka – Taifa Leo

Published

on


Upweke wajaa Ford Kenya Olago naye aking’oka

NA CHARLES WASONGA

MUSTAKABALI wa chama cha Ford Kenya uko hatarini kufuatia idadi kubwa ya wanachama wake wanaokihama na kujiunga na vyama pinzani.

Wiki jana, chama hicho kinachoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula kilimpoteza Mbunge wa Kisumu Magharibi Olago Aluoch ambaye amekuwa nguzo yake katika eneo la Luo Nyanza.

Eneo hilo ni ngome ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye ametangaza kuwa atawania urais kwa tiketi ya muungano wa Azimio la Umoja.

Katika hatua iliyoashiria kujipanga kwa ajili ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa Agosti, Bw Aluoch aliamua kujiunga na chama kipya cha Democratic Alliance Party (DAP-K).

Chama hicho kinachohusishwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, kimetangaza wazi kwamba kitajiunga rasmi na Azimio la Umoja na kumuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Kwenye mahojiano na “Jamvi la Siasa” Bw Aluoch ambaye ni wakili, alisema amefikia uamuzi huo baada ya Bw Wetang’ula kuonyesha kuwa anasongea karibu na chama cha United Democratic Alliance (UDA).

“Niligundua kuwa Wetang’ula anaelekea kujiunga na UDA. Na kwa kuwa sitaki kuhusishwa na mpango huo, nimeamua kujiunga na DAP- K kwa sababu kina sera zinazofanana na Ford Kenya,” akasema.

Bw Aluoch alisema Bw Wetang’ula aliharibu sifa za Ford Kenya pale kundi la wanachama walipoitisha Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) mwaka jana kujadili mienendo yake.

“Hii ndio maana wanachama wa Ford – Kenya wasioridhika na mienendo ya Wetang’ula walibuni chama cha DAP-K ili waunge mkono Azimio la Umoja chini ya uongozi wa Raila Odinga,” akasema mbunge huyo anayehudumu muhula wa pili.

Bw Aluoch anarejelea hatua ya Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi na mwenzake wa Tongaren Eseli Simiyu ambao mwaka jana waliendesha uasi dhidi ya Bw Wetang’ula.

Vile vile, wakati mmoja, wawili hao walijaribu kumng’oa mamlakani Seneta huyo wa Bungoma lakini mahakama ikawawekea kizingiti.

Ni baada ya mipango yao kukosa kutimia ambapo mapema mwezi huu walihama Ford Kenya na kujiunga na chama DAP-K kisha wakatwika wajibu wa kukiongoza.

Chama hiki kimegeuka mwiba kwa Ford Kenya haswa katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia ambako kimekuwa na ufuasi mkubwa kwa zaidi ya miaka 20.

Bw Wamunyinyi juzi aliwaambia wanahabari kuwa DAP-K itafungia Ford Kenya katika kaunti hizo mbili kwa kushinda viti vyote vitano kuanzia ugavana hadi udiwani.

Wengine waliotoroka Ford Kenya hivi majuzi ni mwanawe mpiganiaji wa uhuru Achieng Oneko, Lwande Oneko, miongoni mwa wanachama wengine 15 kutoka kaunti za Bungoma na Trans Nzoia.

Bw Oneko alikuwa anashikilia wadhifa wa mkurugenzi wa Masuala ya Ndani katika Ford –Kenya.

Chama hiki ambacho ni ya pili kwa ukongwe nchini Kenya, baada ya Kanu, ni mojawapo ya vyama tanzu katika muungano, unaoyumba, wa One Kenya Alliance (OKA).