Connect with us

General News

Viongozi wataka Gachagua akamilishe miradi Mt Kenya – Taifa Leo

Published

on


Viongozi wataka Gachagua akamilishe miradi Mt Kenya

NA JAMES MURIMI

VIONGOZI wa Jubilee ambao walipoteza katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, sasa wanataka Naibu Rais Rigathi Gachagua ahakikishie wakazi wa Mlima Kenya kuwa, ujenzi wa barabara kuu ya Mau Mau utakamilika.

Mradi huo ukikamilika utarahisisha usafiri baina ya kaunti za Nyeri na Nyandarua na kuimarisha biashara kati ya wakazi wa kaunti hizo mbili.

Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Bw Kanini Kega, ambaye alipoteza kiti cha ubunge wa Kieni, na Bw Githigaro Wachira ambaye alibwagwa katika kinyang’anyiro cha eneobunge la Tetu, waliahidi kumuunga mkono Bw Gachagua kuwa msemaji wa kisiasa wa Mlima Kenya iwapo atatumia wadhifa wake kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.

Naibu Rais Rigathi Gachagua akihutubia wananchi mjini Nyeri hivi majuzi. PICHA | JOSEPH KANYI

Wakizungumza katika maeneo tofauti, wanasiasa hao wawili walisema kuwa iwapo ujenzi wa barabara hiyo ya kilomita 54 – inayounganisha Ihithe katika eneobunge la Tetu na Ndunyu Njeru kule Kipipiri, Nyandarua – utakwama maendeleo ambayo wakazi wanakusudia kupata yataathirika.

“Tunaunga mkono Bw Gachagua na kuja kwetu pamoja ni kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu. Hiyo ndiyo maana tunazungumza kwa sauti moja ili miradi, kama vile barabara ya Mau Mau, ikamilike,” alieleza Bw Kega ambaye pia ni mkurugenzi wa uchaguzi katika chama cha Jubilee.

Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi wa Barabara Nchini (KENHA) ilitangaza kuwa ilifuta kandarasi ya ujenzi wa barabara hiyo baada ya kukosa kupata idhini kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Mazingira Nchini (NEMA), Shirika la Huduma za Wanyamapori (KWS) na Shirika la Misitu Nchini (KFS).

“Nafikiri kulikuwa na changamoto mbalimbali lakini kama viongozi wa Mlima Kenya lazima tuzungumze kwa sauti moja ili barabara hiyo imalize kujengwa. Uchaguzi umeisha na lazima sasa kama eneo, tupate mgao wetu bila kujali mrengo ambao tulikuwa wakati wa kampeni,” akaongeza Bw Kega.

Kwa upande wake, Bw Wachira alisema kuwa kukamilishwa kwa ujenzi wa barabara hiyo kutafungua miji ya mashambani katika kaunti hizo mbili, huku akiwarai wakazi wapande miti kwa wingi.

“Hii barabara ni muhimu sana katika kufungua Mlima Kenya kimaendeleo ndiposa lazima tuwe na umoja kati yetu. Kaunti ya Nyandarua imekuwa ikizalisha bidhaa nyingi kutokana na kilimo ila hakuna njia rahisi ya kufikia na kusafarisha bidhaa hizo. Kaunti zetu 10 za Mlima Kenya zinastahili kuwa na miundomsingi bora,” akahoji Bw Wachira.Source link

Comments

comments

Facebook

Trending