Wandani wa Uhuru walia kukosa njia
Na MWANGI MUIRURI
KIMYA cha Rais Uhuru Kenyatta kuhusu mwelekeo wa siasa za 2022 kimetia wasiwasi wandani wake katika eneo la Mlima Kenya umaarufu wa United Democratic Alliance (UDA) unapoongezeka.
Mnamo Alhamisi, mwaniaji wa UDA alimshinda mwenzake wa Jubilee katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kiagu, Kaunti ya Meru.
Wanasiasa wanaoegemea mrengo wa handisheki baina ya Rais Kenyatta na Raila Odinga, wanasema Rais Kenyatta hajatimiza ahadi aliyotoa kwamba angetoa mwelekeo wa kisiasa mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.
Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Murang’a, Bi Sabina Chege anasema Rais Kenyatta amewaacha wandani wake katika hali ya sintofahamu.
“Hii shida yote tuko nayo kwa sasa inatokana na kukosa kujipanga kwetu mapema. Uchaguzi wa 2022 umebisha hodi na rais hajatoa mwelekeo. Inaonekana kila mwanasiasa ameanza kujipanga kivyake mapema tukingoja mwelekeo,” akasema.
Bi Chege alisema kuwa tayari yeye pamoja na Mbunge wa Kieni Kanini Kega wameamua mapema kuunga mkono Bw Odinga, lakini bado hawajui kwa uhakika iwapo kinara wa ODM ndiye chaguo la Rais Kenyatta.
“Sasa tuko njia panda kwa kuwa kila uchao wapinzani wetu katika mrengo wa Naibu Rais William Ruto wanaonekana kupiga hatua kubwa Mlimani. Tunahitajika kujibu mapigo la sivyo tutazama,” asema Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu.
Bw Wambugu alisema kuwa wasiwasi huo unajidhihirisha katika visa vya baadhi ya waliokuwa wafuasi sugu wa handisheki kujiunga na UDA au vyama vidogo kwa hofu ya kupoteza viti katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mbunge wa zamani wa Gatanga, Peter Kenneth sasa anamtaka Rais Kenyatta kutaja msemaji wa eneo la Mlima Kenya.
“Wakati wa kutoa mwelekeo ni sasa. Tunafaa kwanza kuandaa mikutano ya kupatanisha Mlima Kenya na tujue mustakabali wetu wa kushirikiana na wengine kwa minajili ya kuunda serikali ijayo. Wakati umewadia wa rais kutupa mwelekeo imara. Tukingoja sana kabla ya rais kutoa mwelekeo wa 2022 wapinzani wetu wataendelea kuwika na kuhadaa wapiga kura wetu, na sisi tutaambulia patupu,” Bw Kenneth alisema majuzi.
Jubilee kufifia
Mbunge wa Kangema, Muturi Kigano naye anaeleza kuwa kwa sasa wapiga kura wa Mlima Kenya wameanza kujifanyia maamuzi, bila kuzingatia ushawishi wa vingozi wa eneo hilo.
“Wasiwasi mkuu ni kwamba sisi bado hatujaamua tuko wapi. Chama tawala cha Jubilee anachokiongoza rais kinazidi kufifia. Uchaguzi wa 2022 nao unakaribia. Wapinzani wetu wa UDA nao wanaonekana kujiimarisha na kutwaa ushindi muhimu katika chaguzi ndogo za hivi majuzi Mlimani,” akasema.
Bw Kigano alisema kuwa kile kinahitajika ni rais awajibikie suala la umoja wa eneo la Mlima Kenya.
“Anafaa ajitokeze na asikilize wapigakura wanataka nini, ili aweze kutupanga. La sivyo, tutajipata mashakani.”
Alisema kuwa hofu ya kuachwa kwenye baridi 2022 imemtia katika njia panda kwani hajui ikiwa ataunga mkono Bw Odinga au Dkt Ruto.
Kwa upande wake, Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui anasema kuwa mrengo wa handisheki haujafanya utafiti wa kutosha kuhusu msimamo wa wapiga kura wa Mlimani.
“Wakati huu ambapo tuko afisini wacha tu tukae kwa rais na mshirika wake wa kisiasa Bw Odinga, lakini kura ikiwadia na kampeni zianze, tujitose ulingoni tukiwa na ufahamu kwamba ni lazima mwaniaji awasikilize wapigakura wa eneo lake,” Bw Kinyanjui anaeleza.
Aliyekuwa mbunge wa Maragua, Kamande Wambuku anasema kuwa aliachana na mrengo wa handisheki baada ya kuhisi kwamba Rais Kenyatta ‘hakuwa na mpango thabiti’ kuhusu urithi wake 2022.
Mwenyekiti wa muungano wa jamii za Gikuyu, Embu na Meru (Gema), Askofu Lawi Imathiu amependekeza kuwa Rais Kenyatta atangaze hadharani kuwa hana nia ya kushawishi urithi wa Ikulu katika uchaguzi mkuu ujao.
“Ingekuwa busara rais akielewa kwamba wimbi ambalo linavuma eneo hili ni la ukaidi dhidi ya kuamuliwa hatima ya kisiasa. Ili kuhepa makabiliano na kuzidisha cheche za kisiasa Mlimani, ningemsihi amalize tu awamu yake na astaafu kwa heshima kwa kuwaachia wapigakura jukumu la kuchagua rais wao na serikali mpya,” akasema Askofu Imathiu.
Kwa sasa, magavana Kiraitu Murungi wa Meru, mwenzake wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki, Mutahi Kahiga wa Nyeri, Nderitu Muriithi wa Laikipia na James Nyoro wa Kiambu ni baadhi ya waliokuwa wametangaza ufuasi kwa mrengo wa handisheki, lakini katika siku za hivi punde wameonekana kulegeza msimamo wakisema kuwa wanashauriana na wapigakura kuhusu mwelekeo wa 2022.
Next article
TAHARIRI: Kongole watimkaji marathon kutuletea sifa tena