Connect with us

General News

Watu 2,600 waaga dunia baada ya tetemeko kutokea nchini Syria na Uturuki – Taifa Leo

Published

on

Watu 2,600 waaga dunia baada ya tetemeko kutokea nchini Syria na Uturuki – Taifa Leo


Watu 2,600 waaga dunia baada ya tetemeko kutokea nchini Syria na Uturuki

NA MASHIRIKA

ADANA, UTURUKI

ZAIDI ya watu 2,600 wamefariki Jumatatu huku maelfu wakijeruhiwa baada ya tetemeko kubwa la ardhi kulikumba eneo la kati nchini Uturuki na kaskazini magharibi mwa Syria.

Tetemeko hilo limebomoa majengo katika maeneo hayo, huku uharibifu huo ukizidisha uharibifu ambao umekuwa ukishuhudiwa katika miji mingi nchini Syria kutokana na vita ambavyo vimekuwa vikiendelea nchini humo kwa miaka mingi.

Tetemeko la kabla ya jua kuchomoza limekuwa la ukubwa wa kiwango cha 7.8 kwenye vipimo vya Ritcher. Na mchana, limetokea tetemeko lingine la kiwango cha 7.7

Limetajwa kuwa tetemeko baya zaidi kukumba Uturuki na Syria katika karne hii.

Wataalamu wamesema ukubwa wake ulihisiwa pia katika mataifa jirani kama Cyprus na Lebanon.

Waokoaji wamekuwa na kazi ya ziada kuwaondoa waathiriwa waliokuwa wamekwama katika mabaki na vifusi vya majengo.

“Tumetikiswa kama kitanda cha mtoto. Tulikuwa watu tisa nyumbani. Wavulana wangu wawili bado wamekwama kwenye vifusi. Ninawangoja,” akasema mwanamke mmoja aliyekuwa amevunjika mkono na kujeruhiwa usoni mwake.

Alikuwa akizungumza kwenye ambulensi karibu na mabaki ya jengo la orofa saba alikokuwa akikaa katika mji wa Diyarbakir, kusini mashariki mwa Uturuki.

Awali, Rais Tayyip Erdogan alikuwa amesema jumla ya watu 912 walikuwa wamethibitishwa kufariki nchini humo 5,383 wakijeruhiwa huku majengo 2,818 yakiharibiwa kabisa. Akasema hangeweza kutabiri jinsi ambavyo idadi ya maafa ingeongezeka, kwani juhudi za uokozi zilikuwa zingali zinaendelea.

Nchini Syria, Wizara ya Afya kwenye takwimu za awali ilikuwa imesema zaidi ya watu 326 walithibitishwa kufariki huku 1,042 wakijeruhiwa. Katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo, ambalo linashikiliwa na waasi, watu 147 waliripotiwa kufariki.

Katika mji wa Diyarbakir, Uturuki, wanahabari wameeleza kuwa mamia ya waokoaji walikuwa wakijaribu kuwatafuta manusura kwenye mabaki ya vifusi vya majengo yaliyobomoka. Katika baadhi ya nyakati, watu waliokwama kwenye vifusi hivyo wameonekana wakiinua mikono ili kuomba usaidizi.

Wanaume kadhaa wamembeba msichana aliyekuwa amefungwa kwa blanketi kutoka kwa jengo lililoharibika katika mji huo.

“Tuliamshwa na mtikiso mkubwa,” akasema Meryem, 29, kutoka mji wa Kahramanmaras, kusini mwa Uturuki.

“Nilikuwa na wasiwasi mkubwa. Nilidhani hali hii haingefikia kikomo. Nilichukua vitu kadhaa vya mtoto wangu wa mwaka mmoja na kuondoka katika jengo hilo,” akaeleza.

Video moja iliyosambazwa katika mtandao wa Twitter imeonyesha majengo mawili yakiangukiana katika mji wa Aleppo nchini Syria. Wakazi wawili katika mji huo wamesema kuwa majengo hayo yalianguka saa kadhaa baada ya tetemeko hilo kufanyika.

Mkurugenzi wa Afya katika mji huo, Ziad Hage, amesema watu waliojeruhiwa walikuwa wakifikishwa hospitalini “kwa mamia.”

Kituo cha televisheni cha serikali nchini humo kimeonyesha vikosi vya uokozi vikiwatafuta manusura huku maafisa wakiwa wamevaa makoti ya kujilinda dhidi ya mvua.

Tayari, zaidi ya nchi 40 zimeahidi kutoa msaada wa kibinadamu kwa waathiriwa.Source link

Comments

comments

Facebook

Trending