Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala ya rambi rambi kwa jamaa, ndugu na marafiki wa Profesa Abel Gitau Mugenda ambaye alifariki jana baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Marehemu Profesa Abel Mugenda ni mumewe Profesa Olive Mwihaki Mugenda, aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kenyatta na pia mmoja wa wanachama wa wakati huu wa Tume ya Huduma ya Idara ya Sheria.
Kwenye risala yake, Rais Kenyatta alisema marehemu Profesa Abel Mugenda alikuwa msomi mwadilifu na mtafiti mashuhuri ambaye kazi yake imechangia vilivyo katika ustawi wa elimu na mafunzo nchini.
Rais alisema marehemu Prof. Mugenda ameandika na kuchapisha vitabu na kazi nyingi za utafiti ambazo zitaendelea kuchangia katika ustawi wa sekta ya elimu nchini kwa miaka mingi ijayo.
“Marehemu Profesa Abel Gitau Mugenda ni mojawapo wa wasomi na watafiti mashuhuri ambao watakumbukwa kwa miaka mingi ijayo kwa kazi yao ya kipekee,” kasema Rais.
Rais alitoa mfano wa mojawapo wa kitabu kilichoandikwa na Profesa Mugenda kiitwacho ‘Social Science Research: Theory and Principles’ ambacho ni muhimu sana kwa muongozo wa utafiti barani Afrika na mataifa yanayostawi.
Rais alisema marehemu Profesa Mugenda alikuwa mzalendo halisi ambaye licha ya ufanisi mkubwa na kujaliwa kupata nafasi nyingine nje ya Kenya, alijitolea kutumikia nchi hii kupitia ujuzi, ufahamu na kipawa chake.
“Bila shaka Profesa Mugenda amewapasha ufahamu muhimu vijana wetu kuhusu mbinu za utafiti sio tu kupitia kuwafundisha bali pia kupitia kazi zake za uchapishaji vitabu. Daima tutamuenzi msomi huyo,” kasema Rais Kenyatta.
Marehemu Profesa Abel Gitau Mugenda amewahi kufanya kazi katika Umoja wa Mataifa na mashirika mengi ya kimataifa yasiokuwa ya kiserikali kama mtaalamu wa utafiti, uchunguzi na ukadiriaji.
Vile vile, Prof. Mugenda amekuwa mhadhiri wa mbinu za utafiti, uchunguzi, ukadiriaji na takwimu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Chuo Kikuu cha Iowa nchini Marekani, Chuo Kikuu cha Kanisa la Methodist hapa nchini na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani kilichoko hapa Kenya (USIU).
Ameandika na kuchapisha vitambu mbali mbali kuhusu mbinu za utafiti ikiwemo kitabu kinachofahamika kama ‘Qualitative Research Methods and Social Science Research: Theory and Principles’.



