Rais Uhuru Kenyatta Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi, alipokea risala ya rambirambi na ya heri njema kutoka kwa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria kufuatia shambulizi la kigaidi wiki hii katika mtaa wa Riverside Drive lililosababisha maafa ya watu 21 na kadhaa kujeruhiwa.
Risala hiyo ya rambirambi na ya heri njema iliwasilishwa na ujumbe ulioongozwa na mjumbe maalumu Profesa Ibrahim Agboola.
Akiwasilisha risala hiyo, Profesa Agboola aliihurumia Kenya akisema Nigeria imekumbwa na matukio kama hayo kufuatia mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram.
“Tunafahamu kile taifa la Kenya inachopitia kwa sababu tunayo hali kama hiyo hiyo nchini mwetu kutokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram,” mwakilishi huyo alisema.
Aliongeza kwamba Rais Muhammadu Buhari na raia wa taifa la Nigeria wanaunga mkono kwa dhati taifa la Kenya kwa katika vita dhidi ya ugaidi.
Vile vile, ujumbe huo ulimuarifu Kiongozi wa Taifa kuhusu maandalizi kabla ya uchaguzi mkuu ujao nchini Nigeria ambapo Rais Buhari anatafuta kuchaguliwa kwa mara nyingine.
Ujumbe huo ulimfahamisha Rais Kenyatta baadhi ya mafanikio yaliyoafikiwa hivi majuzi na Rais Buhari ikiwemo vita dhidi ya ufisadi, vita dhidi ya kundi haramu la Boko Haram na mabadiliko ya kiuchumi ya taifa hilo la Afrika Magharibi.
Rais Kenyatta alipokea risala hiyo ya heri njema na kumpongeza Rais Buhari na raia wa Nigeria kwa moyo huo wa undugu.
Rais alisema kwamba Nigeria na Kenya zinafanana kwa mambo mengi akidokeza kuwa hivi sasa mataifa haya mawili ya Afrika yameathirika na yamo katika harakati za kupigana na maovu mawili ya ufisadi na ugaidi.
“Vita dhidi ya ufisadi husababisha kupoteza marafiki na kuongezeka kwa maadui, hata hivyo sharti vita hivyo vifanikiwe iwapo watu wetu watakuwa na maisha bora,” kasema Rais Kenyatta.
Aliongeza kwamba yatakuwa manufaa makubwa kwa Bara la Afrika wakati vita dhidi ya ufisadi na ugaidi vitakapofanikiwa nchini Kenya na Nigeria.
Mfanyi biashara Alhaji Mohammed Indimi aliyendamana na Mjumbe huyo maalum pamoja na Balozi wa Nigeria hapa nchini Balozi Shiedu Omeiza Momoh walimpongeza Rais Kenyatta kwa juhudi zake za kuhakikisha mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini Kenya.
Katibu Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni Balozi Macharia Kamau alihidhuria hafla hiyo.



