Wednesday, 10 June 2026
Kenyan Digest

Azimwa na korti kunyima dada zake urithi wa baba – Taifa Leo

Staff
3 min read
Published 18 March 2022

Azimwa na korti kunyima dada zake urithi wa baba

NA BRIAN OCHARO

MAHAKAMA inayoshughulikia kesi za kifamilia mjini Mombasa, imeamua kuwa watoto wa jinsia zote wana haki ya kurithi mali ya wazazi wao.

Katika uamuzi uliotolewa na Jaji John Onyiego, suala la iwapo mtu ni mwanamke au mwanamume, halifai kutumiwa kama msingi katika ugavi wa mali ya wazazi.

“Ugavi wa mali unafanywa kisheria kwa watoto, wanandoa au mtegemezi mwingine yeyote. Suala la jinsia halina msingi,” akasema jaji huyo.

Alikuwa akitoa uamuzi huo katika kesi ambapo mwanamume alielekea kortini kuwazuia dada zake kurithi mali ya familia iliyoachwa na marehemu baba yao.

Bw Peter Tole Kiwinga, alitaka kuwazuia dada zake kurithi mali ya baba yao akidai kuwa, katika mila ya jamii ya Wataita, jinsia ya kike haina haki ya kurithi ardhi kutoka kwa wazazi wao.

Bw Kiwinga alikuwa ametofautiana na kaka zake wengine wawili kuhusu iwapo dada zao pia walistahili kunufaika na mali iliyoachwa na marehemu baba yao.

Huku kaka zake wengine watatu wakitaka dada zao pia wanufaike na mali hiyo , iliyopo katika Kaunti Ndogo ya Wundanyi, Kaunti ya Taita Taveta, Bw Kiwinga alipinga hilo akidai kuwa hawakustahili kupewa ardhi kwa sababu wao ni wa jinsia ya kike.

“Mila ya Wataita hairuhusu mtoto wa kike kurithi mali kutoka kwa mzazi aliyefariki,” alisema katika mawasilisho yake kortini.

Wakati huo huo, Bw Kiwinga pia alisema kuwa yeye ndiye mtoto pekee wa mke wa kwanza wa marehemu, hivyo basi alipaswa kupata sehemu kubwa kuliko watoto wengine ambao wote walizaliwa na mke wa pili wa marehemu.

Kesi hiyo iliwasilishwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2018, ambapo ndugu hao wanne walikuwa wakizozana kuhusu usimamizi na ugavi wa mali ya baba yao, marehemu Erasto Kiwingia Tole.

Baada ya kupitia ushahidi uliotolewa katika kesi hiyo, mahakama katika uamuzi wa Novemba 25, 2020 ilipata kuwa watoto wa kiume wa marehemu, walipokea hisa zao kutoka kwa baba yao kama zawadi alipokuwa angali yu hai.

Mahakama pia iliamua kuwa mabinti hao walikuwa na haki ya kurithi mali ya baba yao kwa hivyo hawafai kubaguliwa kwa sababu ya jinsia.

Kwa sababu hiyo, mahakama iligawa mali hiyo kwa mabinti hao. Hata hivyo, Bw Kiwinga hakuridhishwa na maamuzi hayo akaamua kuyapinga katika mahakama ya rufaa.

Katika rufaa yake, alitaka agizo litolewe kuwa, dada zake hawakuwa na haki ya kurithi mali.

Pia alitaka mahakama kusitisha utekelezaji wa uamuzi wa awali ulioruhusu dada zake kurithi mali ya marehemu baba yao.

Alitaka uamuzi huo usitishwe kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa rufaa hiyo. Vile vile, aliomba kuongezewa muda wa kuwasilisha stakabadhi zake za rufaa.

Bw Kiwinga alieleza kuwa alishindwa kuwasilisha rufaa hiyo kwa wakati kwa sababu alikuwa mgonjwa.

Pia alidai kuwa wakili wake amekuwa akiugua kwa hivyo hakuweza kuwasilisha rufaa hiyo ndani ya muda unaotakiwa.

Hata hivyo, Jaji Onyiego alisema sababu ya kuchelewa kuwasilisha rufaa haikueleweka wazi.

“Hakukuwa na ushahidi kuwa mlalamishi na wakili wake walikuwa wagonjwa hadi hawangeweza kuwasilisha rufaa kwa wakati unaofaa.

Kuna sababu mahakama ilipeana siku 30 za kukata rufaa,” akasema jaji huyo. Kwingineko, upande wa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), umepigwa jeki katika kesi inayomwandama wakili Paul Gicheru.

Hii ni baada ya mahakama kukubali ombi la kujumuisha baadhi ya taarifa za mashahidi waliokuwa katika kesi ya Naibu Rais William Ruto, kama ushahidi kwenye kesi hiyo mpya inayoendelea.

Bw Gicheru anadaiwa kuhusika katika mpango wa kushawishi mashahidi kujiondoa katika kesi ya Dkt Ruto, hali iliyodaiwa ilichangia kesi hiyo kufifia hadi ikasitishwa.

Jaji Miatta Maria Samba, anayesikiliza kesi hiyo, pia amekubali stakabadhi mbalimbali za kisheria, taarifa za habari, rekodi za sauti miongoni mwa hati nyingine kutumiwa kama ushahidi dhidi ya Bw Gicheru.


About the author