Wednesday, 10 June 2026
Kenyan Digest

Bunge la sasa limejaa vikaragosi tofauti na watangulizi wao waliojaa hekima – Taifa Leo

Staff
1 min read
Published 1 January 2022

WANDERI KAMAU: Bunge la sasa limejaa vikaragosi tofauti na watangulizi wao waliojaa hekima

Na WANDERI KAMAU

KWA kizazi kilichofanikiwa kufuatilia mijadala ya Bunge la Kitaifa katika miaka ya ‘80 na ‘90, ni wazi iliendeshwa kwa hekima na utaratibu wa aina yake.

Bunge lilikuwa jumba lililoheshimika na kila mmoja. Wabunge walionekana kuwa watu muhimu katika jamii, kiasi hata cha wengine wao kuwatia baridi baadhi ya maafisa wenye ushawishi serikalini.

Michango na utendakazi wa wabunge wa kizazi hicho ndio unaosifiwa kuleta mageuzi ya kiutawala tunayofurahia hadi leo.

Ninarejelea kizazi cha wanasiasa wakongwe kama James Orengo, Koigi wa Wamwere, marehemu Chelagat Mutai, Mwachengu wa Mwachofi miongoni mwa wengine wengi.

Kutokana na ujasiri wao katika kuikosoa serikali na kuwatetea wananchi, walipewa msimbo wa The Seven Bearded Sisters (Ndugu Saba Wenye Ndevu) na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wakati huo, Bw Charles Njonjo.

Ingawa Katiba ya sasa imelikweza Bunge na kulipa mamlaka makubwa ikilinganishwa na miaka ya hapo awali, kizazi cha wabunge wa sasa kimewasaliti wananchi.

Kinyume na awali, ambapo Bunge lilionekana kuwa jukwaa la kuwatetea raia, sasa limegeuzwa uwanja wa fujo, mizaha na ubinafsi usioisha.

Kizazi cha wabunge wa sasa kimejaa watu wenye mizaha, ambapo wakati mwingine, huwa inashangaza jinsi walivyofaulu kuingia bungeni.

Katika bunge la awali, ilikuwa vigumu kuwaona wabunge wakifarakana hadharani, kutusiana au kurushiana makonde kwa misingi ya tofauti zao za kisiasa.

Badala yake, walitofautiana kwa hekima—kupitia hoja nzito zilizowasilishwa kwa njia iliyowavutia hata wakosoaji wa kila upande.

Ni vikao vilivyoshuhudiwa wakati wa maspika kama Francis Ole Kaparo na Kenneth Marende.

Wakati tofauti na majibizano yalipofikia upeo, maspika hao walikuwa wakitumia busara kutoa maamuzi yaliyomridhisha kila mmoja. Wito wetu kwa wabunge ni kuwaiga watangulizi wao, ili kuondoa baadhi ya taswira za kutamausha zinazoshuhudiwa kwa sasa.

[email protected]

NYOTA WA WIKI: Bukayo Saka


About the author