Dallas Allstars yateleza gozi la Koth Biro likipamba moto
Na JOHN KIMWERE
MABINGWA watetezi kwenye mechi za Koth Biro, Dallas Allstars walidungwa na Digo United bao 1-0 kwenye patashika iliyopigiwa ugani Umeme Ziwani, Nairobi.
Kwenye mechi hiyo ya Kundi H, bao hilo lilifunikwa kimiani na David Mlami kunako dakika ya 30.
”Tumeanza mechi zetu vibaya ambapo itabidi turekebishe makosa yetu ili kujiweka vizuri kwenye kampeni za kutetea taji la mwaka huu,” kocha wa Dallas Stephen Mbogo alisema na kutoa wito kwa wachezaji kutolaza damu kwenye mechi zijazo.
Kwenye matokeo mengine ya kipute hicho, James Mandela na Musa Salim kila mmoja, walitikisa wavu mara moja na kubeba Borussia FC kuzoa ufanisi wa mabao 2-0 dhidi ya Life and Sports Academy FC.
Kwa mara ya kwanza ngarambe ya mwaka huu 2021 inadhaminiwa na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga.
Mashindano ya mwaka huu yamevutia timu 46 ambazo zimegawanywa kwa makundi manane.
Dallas Allstars ilishinda taji hilo ilipozaba Ruaraka Allstars kwa mabao 8-7 kupitia penalti baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida mwaka 2020.
Mshindi wa kipute cha mwaka huu atapokea zawadi ya Sh300,000 huku nambari mbili akituzwa Sh100,000 nao nambari tatu na nne watatia mfukoni Sh50,000 na Sh20,000 mtawalia.



