Kidero ahepa korti na kwenda kwenye mkutano wa Azimio
Na RICHARD MUNGUTI
ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero anayekabiliwa na kesi ya ufisadi wa Sh68 milioni jana alihudhuria hafla ya Azimio la Umoja katika uwanja wa Kasarani badala ya kufika kortini kesi hiyo ilipotajwa.
Mbali na Dkt Kidero pia wakili James Orengo anayemwakilisha hiyo pia hakufika kortini kuhudhuria hafla hiyo. Bw Orengo alimtuma wakili Aulo Soweto kueleza hakimu mkuu Felix Kombo hawatafika kortini. Hata hivyo Bw Kombo alisema kesi hiyo ilikuwa imeorodheshwa kutajwa washtakiwa kuifahamisha mahakama ikiwa wamekabidhiwa nakala za mashahidi.
Bi Soweto alieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka haujawakabidhi nakala zote za mashahidi. “Tumepewa nakala chache za ushahidi. Bado zijapokea nakala muhimu nne,” alisema Bi Soweto. Pia Bi Soweto alisema kuna ushahidi ambao upande wa mashtaka umekataa nao na kusema “hawatawapa.”
Kiongozi wa mashtaka Bw James Kihara alieleza mahakama hajapokea barua ya malalamiko kutoka kwa Bi Soweto akieleza matatizo aliyokumbana nao. “Naomba Bi Soweto aandike barua akieleza ushahidi ambao hajapokea ndipo apewe,” alisema Bw Kihara.
Kidero ameshtakiwa kulipa kinyume cha sheria zaidi ya Sh68 milioni kutoka akaunti za kaunti ya Nairobi. Dkt Kidero ameshtakiwa pamoja na aliyekuwa msimamizi wa wafanyakazi George Wainaina, Bw George Wainaina. WengineNg’ang’a Mung’ai, Charity Ndiritu, Peterson Njiru, Ekaya Alumasi, James Mbugua, Elizabeth Nderitu, Alice Njeri na John Wainaina.
Bw Kombo aliamuru Dkt Kidero akabidhiwe nakala zote za ushahidi na kuorodhesha kesi hiyo kutajwa Januari 21,2022.



