Mzee Kibor, mwenyekiti wa kongamano la wanaume, alikuwa na bidii ya mchwa
NA FRED KIBOR
MZEE Jackson Kibor, mkulima maarufu kutoka Uasin Gishu aliyegeuka mwanasiasa ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 88, kutokana na kile ambacho familia ilitaja kama matatizo ya muda mrefu ya Covid-19.
Kulingana na mmoja wa binti zake, Loice, Mzee Kibor alipatikana na maradhi ya figo mapema mwezi huu na amekuwa akipokea matibabu hadi alipoaga dunia Jumatano.
Mzee huyo alifariki dunia katika Hospitali ya St Luke Orthopedic and Trauma iliyopo Eldoret ambapo alilazwa wiki moja iliyopita.
“Aliambukizwa Covid-19 mnamo Oktoba 2020 ambapo mapafu yake yaliathirika vibaya na tangu wakati huo amekuwa akitibiwa,” alisema binti yake marehemu.
Familia hiyo ilifichua kuwa mwen – dazake amekuwa akisafiri na mtu wa oksijeni ambao ulikuwa kando yake kila mara hata ndani ya gari lake.
Mwenye bidii
Alimwelezea baba yake kama mzee mnyenyekevu na mwenye bidii aliyeinuka kutoka hali duni kifedha na kujenga himaya ya kumezewa mate.
Maishani mwake, Mzee Kibor, aliyetwikwa hadhi ya utani kama Mwenyekiti wa Kongamano la Wanaume aliibua hisia za upendo na chuki kwa usawa.
Katika matukio yaliyoandamana upesi, alimpa talaka mke wake wa pili na wa tatu wakifuatana, akawashtaki watoto wake kwa kuingilia mali yake bila idhini na hata kumfyatulia risasi mwanawe, ambayo ni baadhi ya sifa zilizozingira maisha ya Mzee Kibor.
Kuna wakati aliwahi kufungua gari lake lililokuwa limefungwa kwa minyororo na askari wa kaunti kwa kukata chuma cha michororo hiyo.
Wakati mwingine, alifunika gari lake na misumari baada ya bunduki yake kutwaliwa.
Aliwahi pia kukaa katika seli za polisi kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi wa kikabila mnamo 2008.
Lakini kilichowastaajabisha wengi ni wakati alipoelekea kortini kudai vipimo vya vifanyiwe wanawe sita aliozaa na mke wake wa tatu Naomi Jeptoo.
Licha ya kuwa na kiwango cha chini cha elimu na kuzaliwa katika umaskini, Mzee Kibor aliinuka na kujijengea himaya ya kuvutia kwenye zaidi ya ekari 4,000 za ardhi katika Kaunti za Uasin Gishu na Trans Nzoia counties, huku akiwa na wake wanne na watoto 27 baadhi yao wanaosomea au kufanya kazi ng’ambo.
“Nilikuwa mwerevu shuleni lakini nilitoka kwenye familia maskini na nilikuwa nikipeleka fito au kuni kama karo ya shule lakini nilipofika Darasa la Tano walisisitiza tulipe pesa ambazo sikuwa nazo na nikaacha shule kwa kukosa sh 3 katika Shule ya Msingi ya Lelmokwo, Kaunti ya Nandi,” alisema katika mahojiano ya awali.
Alifichua kwamba hakuwahi kum – wona baba yake na kwamba mama yake aliaga dunia akiwa na umri wa miaka sita.
Alihamia katika Kaunti ya Uasin Gishu ambapo alianza kukusanya magamba ya miti na kuiuza katika Kiwanda cha Ngozi cha Eldoret kilichosambaratika kwa sababu hakuwa na tiketi ya ajira.
“Baada ya kufanya kazi hapo kwa miaka kadhaa, nilijifunza kisiri jinsi ya kuendesha lori za kampuni hadi nilipopatiwa idhini,” alisema.
Aliondoka kiwanda hicho cha ngozi na kuanza kuendesha malori ya marehemu milionea Jonathan Kibogy kutoka Uasin Gishu na mwanamme mwingine tajiri kutoka Chepkorio aliyefahamika kama Mz Chirchir Masit.
Alikuwa akinunua gunia la viazi kwa Sh6 kutoka maeneo ya Chepkorio na Metkei na kulipa Sh3 kwa mawakala na wasafirishaji.
“Nikiwa Kampala nilikuwa ninauza kila mfuko Sh16. Nilikuwa nikiweka akiba ya faida ambayo nilitumia kujinunulia lori yangu ya kwanza na nyingine punde baadaye,” alisema katika mahojiano hayo.
Alizunguka kote Afrika Mashariki akitumia trela zake huku akiuza viazi na kusafirisha mahindi kwa kutumia treni ya mizigo kutoka maeneo ya Kipkabus na Ainabkoi.
“Nilikopa Sh55, 000 kutoka Land Bank na kuongeza Sh35, 000 za ziada ambapo nilinunua ardhi yangu ya kwanza yenye ekari 840 eneo la Kipkabus
ambapo nilikuza mahindi na kufuga ng’ombe wengi wa maziwa. Mke wangu wa kwanza Mary ambaye sasa ni marehemu alinisaidia kuendesha ardhi hiyo na kulipa mkopo kabla ya kumwoa Josephine mnamo 1965 aliyeishi vilevile kwenye ardhi hiyo,” alisimulia Mzee Kibor.
Alinunua kipande chake cha pili cha ardhi chenye ekari 1 600 eneo la Kabenes kwa Sh220, 000 mnamo 1969 kabla ya kununua ekari nyingine 1200
mjini Kitale zilizokuwa na ng’ombe 500 wa gredi wa maziwa kwa Sh1.5 milioni na ekari nyinginezo 400 eneo la Moiben kwa Sh12 milioni.
Siasa
Mzee Kibor alijitosa kwenye tasnia ya siasa humu nchini ambapo mnamo 1974 alichaguliwa kama Diwani wa Wadi ya Kipkabus ambapo alihudumu kwa muhula mmoja kabla ya kuhamia Wadi ya Soy ambapo alichaguliwa mara tatu mtawalia.
Hata hivyo, safari yake ya kuinuka kutoka maisha ya umaskini hadi utajiri imegubikwa na mivutano ya ndoa iliyojawa na machungu iliyoishia na mzee huyo mkongwe kuwataliki mabibi zake wa pili na wa tatu, Josephine Jepkoech na Jeptoo mtawalia kwa madai ya kutelekezwa, kudhulumiwa kimwili, ukatili na kunyimwa haki za ndoa.
Alikuwa anaishi na mke wake mchanga Yunita Kibor.
Mkulima huyo mkongwe mnamo Mei 2021 aliamua kubatizwa katika hatua aliyosema ilidhamiriwa kuimarisha uhusiano wake na muumba akisema ilikuwa “maandalizi kwa tukio lolote ambalo lingeweza kuzuka.” Mzee Kibor alikumbatia dini ya Kikristo alipobatizwa kwenye kidimbiwi cha kuogelea cha Hoteli ya Boma Inn Eldoret alipokuwa ameandamana na mke wake, baadhi ya watoto wake na marafiki wachache wa karibu.
Askofu aliyestaafu wa Kanisa la Kianglican (AIC) Silas Yego aliongoza ibada ya ubatizo na kumsifu mzee huyo na familia yake kwa hatua hiyo ya kijasiri.
Next article“Ingawa sikuwa nimebatizwa, mimi ni Mkristo na mfuasi wa dhati wa kanisa la AIC. Sababu ya pili iliyonifanya kuamua kuchukua hatua hii ni kwamba ni sharti tuwe tayari, kila wakati kwa sababu hatujui wakati wako wa kuondoka dunia hii utakapowadia na sitaki kubahatisha kitu chochote au kukiacha kikiwa hakijakamilika. Ninapaswa kubatizwa na kuwa tayari,” alisema.



