Real Madrid wakung’uta Granada na kurejea kileleni mwa jedwali la La Liga
Na MASHIRIKA
REAL Madrid walirejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kusajili ushindi wa 4-1 dhidi ya Granada.
Mabao kutoka kwa Marco Asensio na Nacho yaliwapa Real uongozi wa mapema kabla ya Luis Suarez kurejesha Granada mchezoni mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Vinicius Junior alifungia waajiri wake bao la tatu katika dakika ya 56 kabla ya Monchu wa Granada kuonyeshwa kadi nyekundu kunako dakika ya 67.
Ferland Mendy alizamisha kabisa chombo cha wenyeji Granada baada ya kufunga bao la nne la Real katika dakika ya 76. Ushindi wa Real wanaonolewa na kocha Carlo Ancelotti uliwawezesha kuruka Sevilla na Real Sociedad kileleni mwa jedwali la La Liga huku Granada wakishuka hadi miongoni mwa vikosi vitatu vya mwisho.
Real sasa wanajivunia alama 30, moja zaidi kuliko Sociedad na mbili mbele ya Sevilla. Atletico Madrid wanafunga mduara wa nne-bora kwa pointi 26.



