Real Madrid yakung’uta Bilbao na kufungua mwanya wa alama saba kileleni mwa La Liga
Na MASHIRIKA
KARIM Benzema alifunga bao la pekee na la ushindi katika mechi iliyoshuhudia Real Madrid wakipepeta Athletic Bilbao 1-0 na kufungua mwanya wa alama saba kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Bao hilo la Benzema ambaye ni raia wa Ufaransa, lilikuwa lake la 17 msimu huu na alilipachika wavuni baada ya kushirikiana vilivyo na Luka Modric katika dakika ya 40.
Bilbao kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane jedwalini kwa alama 20 baada ya kutoshinda mechi yoyote kati ya sita zilizopita. Kwa upande wao, Real wamejizolea alama 36, saba kuliko mabingwa watetezi Atletico Madrid na Real Sociedad. Sevilla wanafunga orodha ya nne-bora kwa pointi 28.
Chini ya kocha Carlo Ancelotti, Real walimiliki asilimia kubwa ya mpira dhidi ya Bilbao na wakaelekeza makombora 17 langoni mwa wenyeji wao.
Benzema ambaye amepachika wavuni mabao 12 ligini kufikia sasa msimu huu, sasa anajivunia magoli 35 kutokana na michuano 46 iliyopita katika mashindano yote ya mwaka huu wa 2021. Ufanisi huo unafanya kufikia rekodi ya ufungaji mabao aliyoiweka mnamo 2019.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO



