Wednesday, 10 June 2026
Kenyan Digest

Usalama barabarani ni wajibu wetu sote – Taifa Leo

Staff
4 min read
Published 26 December 2021

MAKALA: Usalama barabarani ni wajibu wetu sote

Na WINNIE ONYANDO

AJALI barabarani hasa msimu wa Krismasi ni suala la jadi ambalo kwa miaka mingi halijapata kusuluhishwa.

Ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) ilionyesha kuwa idadi ya vifo vya ajali barabarani katika muda wa miezi 11 ilikuwa 4,347, ikilinganishwa na mwaka 2020 ambapo watu 3,340 walipoteza maisha yao.

Mwezi Novemba, basi la shule lilitumbukia kwenye mto Enziu huko Mwingi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 30.

Hata hivyo idadi hizo zinatia wasiwasi kwa kuwa inasambaratisha juhudi zilizofanywa kwa miaka mingi na taasisi mbalimbali za kuhamasisha kuhusu usalama barabarani kama njia ya kupunguza idadi ya ajali hizo.

Japo lawama nyingi zinaelekezwa kwa madereva na wanaotumia barabara, idara ya polisi wa trafiki ambayo inakusudiwa kuthibiti hali ya trafiki na kuwaelekeza watu kufuata kanuni hizo pia ni wa kulaumiwa.

“Sababu kuu za ajali hizo ni mwendo wa kasi, kuvuka barabara bila kuwa mwangalifu, kuendesha gari ovyo, utovu wa nidhamu barabarani, ulevi na uchovu hasa miongoni mwa madereva wa masafa marefu,” ikasoma ripoti ya NTSA.

Sheria ya Barabara nchini iliundwa mwaka wa 2007 na hata serikali kuunda mamlaka tatu za utekelezaji wa barabara (Mamlaka ya Barabara Kuu ya Kenya, Mamlaka ya Barabara za Vijijini Kenya na Mamlaka ya Barabara za Mijini ya Kenya).

NTSA kusajiliwa

Pia kuna NTSA, ambayo ilianzishwa 2012 ili kusajili na kutoa leseni kwa magari, madereva na shule za udereva, na kuunda sera za kukuza usalama barabarani.

Utekelezaji wa sheria, hata hivyo, umekosekana, haswa katika sekta ya uchukuzi wa umma huku baadhi ya madereva wa matatu wakikiuka kanuni hizo zilizoanzishwa mnamo 2004.

Sheria zilizopuuzwa zaidi ni zile zinazohitaji magari ya utumishi wa umma kuweka vidhibiti mwendo na abiria kufunga mikanda kila wakati.

Kwa sababu ya uzembe wa utekelezaji, idadi ya vifo katika ajali za barabarani imeongezeka.

Takwimu rasmi zinaonyesha usajili wa kila mwaka umeongezeka maradufu katika miaka mitano hadi kufikia 252,601 ikilinganishwa na takwimu za 2016 za 123,539.

Pikipiki ni za bei nafuu, zinauzwa kati ya Sh65,000 na Sh130,00, hivyo kuwawezesha vijana wengi kuzipata kwa ajili ya biashara.

Mwaka huu, waendeshaji bodaboda wengi wamepoteza maisha yao barabarani kwa kuwa baadhi yao hawana ujuzi unaohitajika katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, msemaji wa serikali, Cyrus Oguna alibaini kuwa magari ya kibinafsi yanaongoza kwa idadi ya ajali barabarani.

Mwaka huu 2021 pekee, takriban watu 1,094 walipoteza maisha yao, hasa katika barabara kuu ya Eldoret kuelekea Nakuru.

Akizungumza Jumanne katika hafla ya kufanya kampeni za usalama barabarani eneo la Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru, Bw Oguna alisema kuwa baadhi ya ajali barabarani zinaweza kuepukika.

“Baadhi ya ajali barabarani zinaweza kuepukika ikiwa madereva watafuata kanuni zote za trafiki. Asilimia kubwa ya ajali hizo hutokea kwa sababu ya uzembe wa madereva,” akasema Bw Oguna.

Kwa upande mwingine, alitoa wito kwa abiria au mtu yeyote apige ripoti ya matukio yoyote barabarani kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kupitia programu ya simu ya NTSA.

“Serikali haitawasamehe mashirika ya magari yanayokiuka kanuni za trafiki. Magari hayo yatakamatwa na leseni zao kuchukuliwa,” akasema Bw Oguna.

Usalama barabarani ni wajibu wa kila mmoja

Watumiaji wote wa barabara wana jukumu muhimu la kutekeleza katika kuhakikisha kuwa kuna usalama barabarani.

Akitoa hamasisho kwa Wakenya kuhusu Usalama barabarani, Bw Oguna alisema kuwa asilimia 95 ya ajali hizo zinaweza kuepukika ikiwa watu watakuwa makini na kujihusisha katika kampeni hizo.

“Magari ya kibinafsi yanaongoza kwa takwimu za ajali barabarani. Huu ni mtindo unaotia wasiwasi sana kwa sababu ajali nyingi hutokea kwa sababu ya tabia za kibinadamu zinazoweza kuzuilika.”

Alitoa wito kwa madereva wote wa magari kuwa waangalifu na kutanguliza usalama barabarani msimu huu wa sikukuu ili kuokoa maisha.

Alisema waendesha bodaboda 1,634 walifariki mwaka huu 2021 kutokana na ajali za barabarani akiwataka madereva kuwa waangalifu na kufuata sheria za usalama.

“Mwaka huu waendesha bodaboda zaidi ya 1,634 walipoteza maisha kutokana na ajali barabarani. Ni msimu wa sherehe na vijana wanafaa kuwa waangalifu wakati huu,” akaonya Bw Oguna.

Sababu zilizochangia ajali mwaka huu

Kulingana na Bw Oguna, sababu kuu za ajali barabarani mwaka huu ni uendeshaji wa magari kwa kasi, kusafiri usiku wa manane, kutotii kanuni za trafiki, magari yanabeba mizigo na abiria kupita kiasi, kuendesha gari bila hati halali, dereva kuendesha gari akiwa na uchovu, kukiuka njia na wakati, magari yasiyofaa barabarani, dereva kuendesha gari akiwa amelewa, kuvuka katika maeneo ambayo hayajabainishwa, kuendesha gari ovyo, na waendeshaji wasio na ujuzi na uzoefu.

“Baadhi ya madereva na haswa waendesha baiskeli hushindwa kuvaa gia za kujikinga kama vile helmeti. Pia hawatumii fulana za kuakisi ili kuongeza mwonekano na kwa ujumla kuendesha ovyo.”

Hatua inazochukua serikali kudhibiti ajali barabarani

Kuna uwezekano serikali itaweza kupambana na ajali barabarani. Kuna baadhi ya hatua ambazo serikali imechukua ili kupambana na ajali hizo.

Kwanza kabisa, NTSA ikishirikiana na Huduma ya Kitaifa ya Polisi imeanzisha mpango wa kuwahamasisha wananchi kuhusu usalama barabarani.

Kando na kuhamasisha umma, kampeni hizo pia zinatoa jukwaa la kuwaripoti madereva wanaofanya makosa kupitia NTSA.

Kadhalika, serikali pia inafanya ukaguzi wa magari kote nchini hasa wakati huu wa Krismasi.

Kwingineko, vijana waliopokea mafunzo kutoka Huduma ya Vijana nchini wanatoa mafunzo ya kipekee kwa waendesha bodaboda kuhusu usalama barabarani.

Serikali pia inarekebisha shule za udereva kote nchini ili kuwaondoa madereva ambao hawana ujuzi hitajika katika sekta hiyo.

Simanzi tele baada ya kifo cha Tutu, 90


About the author