Wednesday, 10 June 2026
Kenyan Digest

Wakazi wa Thika wahimizwa kuchukua kura – Taifa Leo

Staff
2 min read
Published 6 February 2022

Wakazi wa Thika wahimizwa kuchukua kura

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika wamehimizwa kujitokeza kwa wingi ili kujisajili wawe wapigakura.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alitoa wito huo hasa kwa vijana ambao wengi wao wanatarajia kuchukua kura kwa mara ya kwanza.

Mbunge huyo yumo mbioni kuwarai vijana wachukue kura ikitiliwa maanani kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilizindua zoezi hilo mnamo Januari 17 huku ikitarajiwa kukamilisha kazi hiyo Februari 6, 2022.

Mbunge huyo alikuwa akizunguka eneo lake ya uwakilishi katika msafara wa lori kubwa mnamo Jumamosi, huku akiwarai wananchi kujiandikisha wawe wapigajikura.

“Iwapo hutajiandikisha inamaanisha kuwa wewe huna sauti ya kujitetea kwa mwakilishi wako. Kwa hivyo ninawarai wakazi wa Thika wajitokeze kwa hizo siku mbili zimesalia,” alieleza mbunge huyo.

Bw Wainaina anajiandaa kuwania kiti cha ugavana Kiambu mnamo Agosti 9, 2022.

“Watu wengi hawakujitokeza kujiandikisha kuchukua kura katika eneo la Thika. Ninawasihi wafanye hivyo haraka iwezekanavyo ili waweze kumchagua kiongozi atakayezingatia maslahi yao,” alifafanua mbunge huyo.

Alieleza kuwa kila mpigakura ana nafasi ya kubadilisha kura yake na kuipeleka kwingineko anakotaka kupigia kura.

Hata hivyo uchunguzi uliofanywa umebainisha kuwa ni watu wachache sana waliojitokeza kujiandikisha wawe wapigakura.

Ilidaiwa kuwa wengi wa vijana hawana vitambulisho vyao huku vikiwa bado kwa vituo vya kuchukulia kadi hizo.

Pia watu wengi wanaonekana hawajachangamkia uchaguzi ujao huku wakingoja kujionea tu na macho yatakayojiri.

Kulingana na rejista ya takwimu za wapigakura, mji wa Thika uliandikisha wapigakura 147,761 mwaka wa 2017.

Kwa muda wa wiki tatu zilizopita makarani wengi wanaoandikisha wapigakura walionekana wakiwa wameketi tu vitini wakingoja watu wa kusajiliwa.

Katika wiki ya kwanza katika wadi tano zilizoko katika mji wa Thika, watu waliojiandikisha ni 1,744.

Hata hivyo inakisiwa kuwa siku ya mwisho mnamo Jumapili watu wengi watafurika katika vituo tofauti ili kujiandikisha dakika za lala salama.

KCAA yasisitizia wanasiasa kuzingatia usalama wa helikopta


About the author