Waziri wa masuala ya Kigeni wa Amerika kuanza ziara Afrika
Na AFP
WAZIRI wa Masuala ya Kigeni wa Amerika Antony Blinken Jumatatu anatarajiwa kuanza ziara yake barani Afrika.
Waziri huyo atatua nchini Kenya Jumatatu na kisha kuelekea Nigeria kabla ya kumalizia ziara yake ya siku tatu nchini Senegal.Wizara ya Masuala ya Kigeni ilisema kuwa Bw Blinken atakutana na marais wa nchi zote, wajadiliane kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo ushirikiano wa kiuchumi.
Taarifa ya wizara hiyo ya Amerika inasema kuwa Waziri Blinken atajadiliana na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu janga la corona, mabadiliko ya tabianchi na mikakati ya ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.
Vilevile, waziri huyo atajadiliana na Rais Kenyatta kuhusu amani katika mataifa ya Ethiopia, Somalia na Sudan.Waziri huyo anakuja barani Afrika mwezi mmoja baada ya Rais wa Amerika Joe Biden Kukutana na Rais Uhuru katika Ikulu ya White House, Washngton DC.
Rais Kenyatta ni rais wa kwanza wa Afrika kukutana na kiongozi huyo wa Amerika katika Ikulu ya White House.Katika mkutano wao, marais hao wawili walizungumzia kuhusu juhudi za kulinda na kuheshimu demokrasia na haki za binadamu kwenye ukanda wa pembe ya Afrika hasa Ethiopia, namna ya kuimarisha uchumi na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Jumanne, Blinken ataelekea jijini Abuja ambapo atakutana na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari kujadili masuala ya ushirikiano katika sekta za afya, usalama, demokrasia na kawi.Atakamilisha ziara yake jijini Dakar, Senegal, ambapo atakutana na Rais Macky Sall na kujadili masuala ya ushirikiano.
Next article


