Connect with us

General News

Were Mukhusia – Taifa Leo

Published

on


GWIJI WA WIKI: Were Mukhusia

Na CHRIS ADUNGO

UTANGAZAJI wa soka ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Michael Were Mukhusia akiwa mwanafunzi wa darasa la sita.

Zaidi ya kuwa shabiki sugu wa ‘Taifa Leo’, alikuwa na mazoea ya kusikiliza KBC na akavutiwa na watangazaji mahiri wa mpira redioni.

Alishiriki tamasha nyingi za muziki na drama akiwa sekondari na majukwaa hayo yakachangia kunoa kipawa chake cha ulumbi. Alitamba kwa wepesi katika uimbaji na uigizaji kutokana na ukubwa wa kiwango chake cha ubunifu na umilisi wa Kiswahili.

Hadi sasa, upekee wake kila anapojipata nyuma ya bomba ni ufundi wa kusana lugha na utajiri wa msamiati unaompa wepesi wa kuita maneno akitangaza mpira.

“Vibarua vya kila sampuli nilivyofanya baada ya KCSE vilinielekeza zaidi katika ndoto iliyokuwa lazima niote – kuwa mtangazaji wa kustahiwa katika ulingo wa kabumbu,” anasema.

Alijitosa katika biashara ya kuuza matunda mjini Kakamega kabla ya kuwa mhudumu wa bodaboda ya baiskeli kisha utingo mjini Kakamega, Bungoma, Mumias na Kisumu. Alifyatua pia matofali na akawa ‘fundi wa mkono’ katika maeneo mbalimbali ya ujenzi.

Were alizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Shikhambi, Kakamega. Alianza safari ya elimu katika chekechea ya Nabongo kabla ya kujiunga na shule za msingi za Kakamega Muslim, Liaranga (Kisii) na Amalemba kisha Kakamega High (1999-2002).

Ana diploma ya utangazaji kutoka Chuo Kikuu cha Multimedia (MMU) na alijiendeleza kitaaluma kwa kusomea shahada ya uanahabari katika Chuo Kikuu cha Nairobi (2012-2015).

Kabla ya kujiunga na KBC kwa mafunzo ya nyanjani mnamo Januari 2011, alikuwa tayari msomaji wa taarifa za habari na mtangazaji wa mpira katika MMU Radio 99.9 FM.

Alikuwa pia mwigizaji katika kipindi cha ‘The Team’ (Citizen TV) na akapata fursa ya kutia sauti kwenye matangazo yaliyopeperushwa katika vyombo vya habari kwa faida ya Baraza la Maaskofu, Kanisa Katoliki nchini Kenya.

Alijiunga na Ukweli Video Productions mnamo Juni 2011 kuwa mpiga picha na mtaalamu wa kuhariri video. Akiwa huko, alikuwa vilevile mtangazaji, mchanganuzi na mwendeshaji wa vipindi vya mpira katika idhaa ya KBC.

Alitamalaki shindano la ‘Bonga Boli’ mnamo 2012 na akaajiriwa na SuperSport kuwa mtangazaji wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) na mechi za soka ya kimataifa. Mbali na kuwa mhadhiri wa MMU (2017-2022), aliwahi kufanya kazi na kampuni za Bamba Sports (2018) na MediaPro (2019) kabla ya kuajiriwa na idhaa ya Kiswahili ya Radio France International (2020-2021).

Were kwa sasa ni mchanganuzi na mtangazaji wa mpira katika runinga ya K24 (Mediamax Network Ltd). Zaidi ya kuchangia makala na video mtandaoni (K24 Plus), anashirikiana na mwanahabari Andenga wa Odinga kutayarisha kipindi ‘Sports Extravaganza’ (Milele FM).

Anachangia pia uendeshaji wa vipindi vya michezo na uchanganuzi wa siasa za Kenya katika redio mbalimbali za Tanzania zikiwemo U-FM 107.3, E-FM 93.7 FM Dar es Salaam, na A-FM 92.9 Dodoma.

Kwa pamoja na mkewe Bi Everlyne Mbeyu, wamejaliwa mtoto wa kike – Zuri Namakhabwa.

“Maisha ni safari. Kuwa na malengo. Yaweke hai matumaini yako. Thamini unachokifanya. Usife moyo. Kuwa na msimamo. Pambana. Mtegemee Mungu,” anashauri.Source link

Comments

comments

Trending