– Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa kumi na moja unusu asubuhi mnamo Jumatano, Januari 1 huku waathriwa wakielekea nyumbani wakitoka kwa sherehe
– Gari hilo liliteleza kutoka barabarani, kugonga daraja na kuanguka kwenye mtaro
– Walifariki papo hapo na miili yao kupelekwa katika hospitali iliyokuwa karibu
Yamkini watu watano wamethibitishwa kufariki baada ya kuhusika kwenye ajali ya gari katika barabara ya Eldama Ravine kuelekea Torongo, kaunti ya Baringo baada ya dereva wa gari walimokuwa wakisafiria kupoteza mwelekeo.
Watano hao walikuwa wanatoka kwa sherehe iliyoandaliwa katika mgahawa wa Taiday ambapo mamia ya wakazi walikuwa wamejumuika kwa kesha ya kukaribisha mwaka mpya wa 2020.
Kulingana na kamanda wa polisi wa Eldama Ravine, Rashid Mohammad, ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa kumi na moja unusu asubuhi mnamo Jumatano, Januari 1, wakati marehemu walikuwa wanaelekea nyumbani.
“Walikuwa wanaelekea nyumbani baada ya sherehe wakati gari lao lilipoteza mweleko, kugonga daraja na kuanguka kwenye mtaro. Ni ajali ya kujitakia,” alisema Mohammad.
Watu wote watano waliokuwa katika gari hilo aina ya Toyota Wing Road walifariki papo hapo.
Haya yanajiri saa chache baada ya maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Usalama Barabarani (NTSA) kunasa gari aina ya Probox likiwasafirisha watoto 15.
Maafisa hao waliwachwa vinywa wazi wakati walisimamisha gari hilo ambalo lilikuwa linatumia barabara ya Meru na kuwapata watoto hao wakiwa wamefinywa pamoja.