ICC: Gicheru apumua ombi la upande wa mashtaka likitupwa nje
NA VALENTINE OBARA
WAKILI Paul Gicheru, aliyeshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa madai ya kuhonga mashahidi, amepata afueni baada ya jaji kukataa ombi la upande wa mashtaka kuhusu shahidi mpya.
Upande wa mashtaka ulikuwa umeomba mahakama kuruhusu nakala za mahojiano ambayo shahidi huyo alifanyiwa awali zitumiwe kortini, kando na kuwa shahidi huyo pia angefika mahakamani mwenyewe kuhojiwa.
Kulingana na upande wa mashtaka unaoongozwa na Naibu Kiongozi wa Mashtaka, Bw James Stewart, ombi hilo lilinuiwa kurahisisha mahojiano ya shahidi ambaye amedaiwa ana changamoto mbalimbali ikiwemo uzee ambao haumwezeshi kukaa kwa muda mrefu, na lugha kwa vile anawasiliana kwa Kiswahili.
Kwa niaba ya Bw Gicheru, wakili wake, Bw Michael Karnavas, aliambia mahakama hiyo inayoongozwa na Jaji Miatta Maria Samba kuwa wanapinga ombi hilo kwa vile walifahamishwa kuchelewa ilhali hayo ni mambo ambayo upande wa mashtaka ulifahamu kwa muda mrefu.
“Inasikitisha kuwa nilipokea ombi hili Jumapli mchana. Huyu ni shahidi ambaye aliwahi kuhojiwa na upande wa mashtaka Machi 2021. Ijapokuwa mahojiano hayo hayakuwa ana kwa ana, ingetambuliwa alikuwa na changamoto kwa hivyo upande wa mashtaka ungewasilisha ombi lake mapema,” akasema.
Alieleza kuwa, ni muhimu mahakama izingatie haki za mshtakiwa katika kesi hiyo.
“Huenda machoni pa wengine kesi hii ni nyepesi ikilinganishwa na nyingine, lakini hii kesi ni nzito kwa Gicheru kwa sababu uhuru wake na taaluma ziko hatarini,” akasema Bw Karnavas.
Jaji Samba akitupa nje ombi la upande wa mashtaka, alikubaliana na Bw Karnavas kuwa mshtakiwa atakosewa haki endapo ombi hilo lingekubaliwa.
“Mshtakiwa alijiandaa kwa shahidi kuwasilishwa ushahidi wake moja kwa moja mahakamani. Haiwezekani kufanywa mabadiliko ombi likiwa limechelewa namna hii,” akasema jaji.
Bw Gicheru anakabiliwa na madai ya kushawishi mashahidi kujiondoa kwa kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 iliyomkumba Naibu Rais William Ruto ambaye alikuwa ameshtakiwa pamoja na mwanahabari Joshua Sang.
Next article
Kajwang’ amshauri Wanjigi akubali kuunga mkono Raila