TAHARIRI: KCPE: Wizara isiharakishe kutangaza matokeo
NA MHARIRI
KATIKA siku za hivi karibuni, serikali, kupitia Wizara ya Elimu imefanya kila juhudi kuhakikisha mitihani ya kitaifa nchini inaendeshwa katika mazingira salama na yanayowezesha wanafunzi kupata alama wanazostahili.
Msururu wa visa vya wizi wa mitihani ambavyo vilitishia kuhujumu uhalali wa vyeti vinavyotolewa na Baraza la Mitihani nchini (Knec) vimepunguzwa maradufu.
Na kwa hilo tunaipongeza serikali, na hasa Waziri wa Elimu, Prof George Magoha.
Hata hivyo, tangazo la hivi majuzi la Prof Magoha kwamba, walimu wanaosahihisha mitihani hiyo wamo mbioni kukamilisha zoezi hilo ndipo matokeo yatangazwe Jumatatu ijayo au Jumanne ni la kushangaza.
Ni kweli kwamba, baraza hilo la mitihani kwa sasa linatumia teknolojia mpya kusahihisha baadhi ya mitihani.
Lakini kuna bado masomo kama insha ambayo yanahitaji mwalimu asome ndipo amweke mtahiniwa kwenye mizani akitumia vigezo vilivyowekwa na wizara hiyo.
Hilo kwa kweli si zoezi ambalo linaweza kuharakishwa.
Kumekuwa na ripoti hapo mbeleni kuhusu walimu wanaolazimika kusahisha mitihani hiyo katika mazingira ya kudhalilisha huku wengine wakifanya kazi hadi usiku wa manane ndiposa wafanikishe makataa waliowekewa na Wizara ya Elimu.
Ukandamizaji wa aina hii haufai.
Tunatambua umuhimu wa kutangaza matokeo hayo kwa wakati unaofaa.
Tunafahamu kwamba, siku za nyuma, kulikuwa na visa vya wakuu wa shule kushirikiana na maafisa katika Knec kuvuruga alama za watahiniwa.
Hata hivyo tunaamini mikakati mbalimbali iliyowekwa wakati wa usimamizi wa Prof Magoha inatosha kudhibiti uhalifu huo.
Tunachohimiza kwa sasa ni kwamba, mchakato mzima wa kusahihisha na kutangaza matokeo uendeshwe kwa namna ambayo haitatia doa wala kuibua hisia za shaka kuhusu uhalali wa matokeo hayo.
Wanafunzi waliofanya mtihani wamesubiri kwa muda mrefu kufanya mitihani hiyo na tunaamini wako radhi kusubiri kwa muda zaidi angalau wapate matokeo ambayo yanasawiri uwezo wao kamili wa kielimu.
Waziri Magoha amefanya kazi nzuri, asikubali kuharakisha kutangaza matokeo ya KCPE, hali ambayo inaweza kumshushia hadhi.
Next article
MAKALA MAALUM: Wakazi wa Turkana kupata maji kaunti…