Mzee aliyesaidia Kenyatta gerezani ataka atambuliwe
NA MAUREEN ONGALA
ASKARI jela wa zamani wa gereza la Kapenguria enzi za ukoloni, Mzee Hussein Buro Mohamed, anataka atambuliwe kama shujaa wa taifa akisema alimsaidia hayati Mzee Jomo Kenyatta alipokuwa kizuizini.
Bw Mohamed, 103, ameeleza jinsi licha ya kuwa mwajiriwa wa utawala wa ukoloni, alijitolea kumsaidia Mzee Kenyatta kuwasilisha jumbe mbalimbali kwa familia yake na wandani wake wa kisiasa kisiri.
Kulingana naye, msimamo wake wa kuchangia katika juhudi za kuletea Kenya uhuru ulimfanya awe mwandani wa Mzee Kenyatta tangu mwaka wa 1952.
Bw Mohamed alizaliwa katika eneo la Modogashe, Kaunti ya Garissa mwaka wa 1919 na akaajiriwa kuwa askari jela akiwa bado kijana.
“Nilipokea mafunzo yangu Lamu kisha nikapelekwa kufanyia kazi wakoloni katika shamba la unyunyuziaji la Hola, baadaye nikapelekwa Nairobi kisha kuwa mlinzi wa wafungwa sita wa Kapenguria,” akaeleza.
Katika gereza hilo, alipewa kazi ya kulinda Mzee Kenyatta na wafungwa wenzake ambao ni Achieng’ Oneko, Bildad Kaggia, Kung’u Karumba, Fred Kubai na Paul Ngei.
Mzee huyo ambaye ni baba wa watoto 20, wajukuu 45 na zaidi ya vitukuu kumi, alieleza jinsi alikuwa akificha barua za wafungwa kisha kupelekea jamaa zao na wandani wao wa kisiasa.
Vile vile, anasema alikuwa akiwapelekea wafungwa hao habari kuhusu yaliyokuwa yakiendelea huko nje, zikiwemo baadhi ya siri za wakoloni.
Alikumbuka jinsi Mzee Kenyatta alivyokuwa akimpa barua ili atafute njia ya kuzipeleka katika bunge la Lancaster. Alikuwa akificha barua hizo katika sare zake.
“Wakati mmoja, wazungu walipata barua hizo wakakasirika. Walitaka niwaambie nani huleta barua hizo gerezani lakini nilikana kufahamu chochote,” akasema.
Kando na kulinda wafungwa Kapenguria, alikuwa pia na kazi ya kutoa ulinzi kwao walipokuwa wakihamishwa kuelekea magereza mengine nchini. Alieleza jinsi wakati mmoja alimpeleka Paul Ngei kwa gereza tofauti.
Wakati aliposhukiwa kuhusika katika kuwasaidia wafungwa, alihamishwa kutoka gereza moja hadi jingine ikiwemo Shimo la Tewa, lakini baadaye akarudishwa Kapenguria.
Kulingana naye, urafiki wake na Mzee Kenyatta uliendelea hata baada yake kuwa rais.
Wawili hao walikutana katika shamba la Mzee Kenyatta eneo la Shimo la Tewa, wakati Bw Mohamed alipokuwa amepeleka wafungwa kufanya kazi katika shamba hilo.
“Alikuwa katika orofa ya juu na kuniona, aliniuliza kwa nini sikuwa nimemtafuta lakini nikamwambia ninahudumia asasi ambayo ilinihitaji niombe ruhusa kwa wakubwa wangu. Mzee alipuuzilia mbali maelezo hayo akaniagiza niwe nikimtembelea. Alinipa Sh3,000 ambazo wakati huo zilikuwa ni pesa nyingi mno, pamoja na vyakula nipelekee familia yangu,” akasema.
Licha ya hayo yote, mkewe, Bi Hawa Hussein, 96, anasema hawajavuna matunda ya ushujaa wa mumewe.
“Hatujatambuliwa na yeyote. Nilikuwa na mume wangu kila wakati hadi tulipopata uhuru na alihatarisha maisha yake akiwa msiri wa wafungwa, lakini tunaishi kama mbwa,” akasema.
Kulingana naye, watoto wao bado hutatizika kupata vitambulisho vya kitaifa hadi leo licha ya kuwa walizaliwa Kenya.
Watoto wao ambao ndio tegemeo lao sasa, walitoa wito kwa asasi za serikali kumtambua baba yao kama shujaa aliyehusika katika juhudi za kuleta uhuru nchini.