Mkasa: Familia ya Okwach bado ina matumaini ya kumpata mpendwa wao
NA KASSIM ADINASI
FAMILIA ya Bw Tom Okwach, aliyezikwa kwenye timbo la dhahabu la Abimbo eneo la Sakwa, Kaunti ya Siaya, bado inaendelea na juhudi za kumtafuta miezi kufikia sasa.
Unapofika eneo hilo, lililo katika Kaunti Ndogo ya Bondo, wachimbaji dhahabu wanaendelea na kazi zao za kawaida, japo kutowekwa kwa Bw Okwach bado kunaonekana kuwasumbua akilini.
Katika mkasa huo mtu mmoja walifariki huku sita wakiokolewa.Juhudi za familia ya Bw Okwach kuomba usaidizi kutoka kwa wadau mbalimbali bado hazijafua dafu.
Hata hivyo, matumaini ya kumpata mpendwa wao akiwa hai au amefariki bado yanaendelea kudidimia.
Ni matumaini hayo ambayo yameendelea kuwaweka kwenye eneo la mkasa kwa muda huo wote.
Kulingana na tamaduni za jamii ya Waluo, wakati mwili wa mtu katika familia unakosa kupatikana, kuna njia ambapo familia hizo huamua kumuaga jamaa yao.
Kulingana na Mzee Daniel Okuku kutoka eneo la Kagan Kanyarwanda, Kaunti ya Homa Bay, moja ya njia hizo ni kuzika mgomba kama ishara ya kumuaga mtu huyo.
Anasema desturi hiyo huwa ishara kwa familia husika kwamba imemzika mpendwa wao.
“Ni mtindo wa kawaida miongoni mwa jamii ya Waluo uliokuwa ukifanywa wakati mtu alifariki akiwa mbali au alipofariki na mwili wake haukupatikana. Jamii ingezika kipande cha mgomba kuridhisha roho ya marehemu ili kutowasumbua walioachwa,” akasema Mzee Okuku.
Aliongeza: “Katika jamii ya Waluo, kaburi huwa na uzito mkubwa sana. Wakati familia inaona kaburi, mawazo yao huwa yanatulia kwani inafahamu kuwa mwenzao anapumzika.”
Shughuli ya kuzika kipande cha mgomba huwa inaendeshwa sawia na utaratibu unaofuatwa kwenye mazishi ya mtu wa kawaida.
Familia hulizunguka kaburi, ambapo taratibu za kawaida ambazo hufanywa katika mazishi, hutekelezewa mgomba uliozikwa.
Njia ya pili ni kuzika jiwe kutoka eneo ambalo marehemu amezikwa mbali na nyumbani, ili kuashiria kaburi lake.
“Huu pia ni mtindo wa kawaida miongoni mwa jamii ya Waluo. Kwa mfano, wakati mtu anafariki akiwa ng’ambo na inalazimika azikwe huko, jiwe kutoka kaburi la ng’ambo alikozikwa hupelekwa nyumbani kwake au kwao mashambani. Baadaye huzikwa kuashiria uwepo wa kaburi lake,” anahoji Mzee Okuku.