-Junet anahusishwa na sakata ya kwanza ya Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS) ambapo KSh1.9 bilioni zilifujwa
-Junet, ambaye ni mshirika mkuu wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga, anasemekana alinufaika na fedha hizo
-Junet alihusishwa na kampuni mbili mnamo 2015, ambazo zilisambaza bidhaa za KSh129 milioni kwa NYS
Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohammed, anachungulia hatari ya kukamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), kuhusiana na sakata ya Shirika la Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS).
Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji tayari kuidhinisha kuendelea kwa kesi dhidi ya watuhumiwa wapya wa sakata ya kwanza ya NYS.
Junet, ambaye ni mshirika mkuu wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga, anasemekana alinufaika na fedha zilizofujwa kama ilivyoripoti gazeti la Taifa leo Jumatatu, Julai 20.
Junet alihusishwa na kampuni mbili mnamo 2015, ambazo zilisambaza bidhaa za KSh129 milioni kupitia kwa zabuni za NYS ambazo ziliibuwa utata.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho na Junet Mohammed walipomtembelea Raila Odinga Dubai akipokea matibabu. Picha:Junet Mohammed. Source: Facebook
Aidha, makachero wa EACC wanachunguza kwa makini zabuni ambayo ilipeanwa kwa kampuni ya Zeigham Enterprises ambapo Junet ni mmoja wa wakurugenzi wakuu pamoja na kaka yake Hussein Mohamed Haji.
Kulingana na uchunguzi wa EACC, kampuni hiyo ilikabithiwa kandarasi ya kusambazia NYS vifaa vilivyogharimu kima cha KSh21.8 milioni.
Makao Makuu ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC). Picha:UGC Source: UGC
EACC inasema kiasi ya pesa za zabuni hiyo zilitumwa katika akaunti ya benki ya Waziri Msaidizi wa Michezo Hassan Noor Hassan, na ya mke wake Meymuna Sheikh Nuh ambaye ni dada yake Junet.
Inadaiwa haya yalitokea wakati Hassan alikuwa akihudumu katika Wizara ya Ugatuzi iliyokuwa ikiongozwa na Anne Waiguru na ndiye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya zabuni iliyochagua kampuni ya Zeigham.
Sakata hiyo inahusisha uporaji wa KSh1.9 bilioni wakati wa muhula wa kwanza wa Rais Uhuru Kenyatta Uongozini.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsaApp: 0732482690.