TALANTA ni muhimu katika maisha na inaweza kukupeleka mbali ukiigundua na kuikuza ili kujinufaisha, na pia kuwanufaisha wengine.
Ni muhimu kujitolea kukuza talanta kwa kila namna. Huu ni mtazamo wa mwanamuziki chipukizi Charles Ochieng, almaarufu Dizo Cappy anayelenga kuwa kiwango cha kundi la Wasafi.
Dizo alilelewa mjini Nairobi na mamake, mzazi pekee katika mazingira magumu ya kiuchumi. Alipogundua kipaji chake cha muziki baada ya kidato cha nne aliamua kuchangamka ili kumpiga jeki mamake.
“Mamangu mzazi aling’ang’ana sana. Aliendesha kilimo na kiduka uchwara kuhakikisha tulipata mahitaji yetu. Nilipogundua kipaji changu cha muziki niliamua kujaribu bahati yangu,” Dizo alisema wakati wa mahojiano.
Ajiunga na kundi la kimuziki la Rogjamaz katika mtaa wa Mathare kwa juhudi za kujiendeleza kimuziki. Kwa kukosa makini na wahusika kuwa na maazimio tofauti, walitengana na kila mmoja akenda zake, lakini hili halikutosha kumkatisha tamaa.
Dizo alianzisha kundi lake la Waarabu Empire katika mtaa wa Mradi, ambalo alijitahidi kulikuza licha ya changamoto tele alizokumbana nazo. Aliwaunganisha vijana na kuwasisitizia umuhimu wa kuungana na kuhemshimiana katika kutimiza malengo yao.
Baadhi ya vijana wa Waarabu Empire. Picha/ Ndungi Maingi
Vijana hawa wanashiriki muziki aina ya ‘Gengetone’, na kuwahusisha vijana katika shughuli za kujijenga.
Ni kundi lenye watu 37 ambao wanapania kunguruma katika sekta ya muziki.
“Tuko jumla ya watu 37, lakini waimbaji ni watatu. Wengine hushirika zaidi katika densi. Ni jukumu la kila mmoja kutafuta pesa kwa mbinu zake tunapotaka kwenda studi. Kil mara nawasisitizia kuwa wakweli na kuheshimiana na tutaenda mbali,” alieleza.
Kwa upande wake, muziki unamhitaji kujikuna ajipatapo na hivyo analazimika kupiga vibarua kupata hela za kwenda studio. Huwa anafanya kazi ya mijengo, umekanika ambao humsaidia rafiki yake Victor(japo hasomea) na yoyote nyingine halali anayopata.
Licha ya kukosa mfadhili, kundi hili linajitolea kwa kila hali, kila mmoja akijitolea kufanikisha sekta yake; wanaoandika nyimbo, wanaochagua midundo na kuimba na wale wa kunengua miili vilevile, hadi hatua ya kutua studioni kutoa kibao.
Dizo alifichua kuwa wakati mwingine alihiari kujihini raha na hata mlo kwa ajili ya talanta yake. Anaamini kuwa Mungu atawapigania na siku moja watafika wanakoenda katika safari yao ya muziki, hasa kwa kuwa dalili za matumaini zimeanza kuonekana.
“Tunapitia magumu mengi lakini hatuwezi kukata tamaa kwani ni kipaji chetu. Lazima tujitolee mhanga kupigania tunachopenda,” alisisitiza.
Kundi lake hushirikisha muziki katika hafla tofauti wanazoalikwa na hili huweza kuwaletea kipato kemkem. Pia nyimbo zinapatikana katika mtandao wa youtube chini ya mada “Odidi Platnumz”.
Msanii huyu pia hupatikana katika mtandao wa Facebook kwa lakabu ‘Dizo Mish’.
Waarabu Empire wamefanikiwa kutoa albamu mbili za muziki kwa majina “Chapa Madem” na “Mawoo”, zikiwa na jumla ya nyimbo 12. Bado nyingine zinaendelea kuandaliwa.
Maudhui ya nyimbo zao aghalabu huhusiana na ugumu wa maisha hasa katika mitaa ya mabanda au “ghetto”, masuala ya mapenzi katika jamii ya sasa na mbinu za kuzoea mabadiliko ya maisha na kukabiliana nayo.
Nyimbo hizi hunuia zaidi kutumbuiza hasa vijana, miongoni mwa malengo mengine. Hivyo basi, huwa na mdundo wenye kutekenya hisia na kusisimua. Huwa hazina mtindo au mdundo maalum, yaani huwa ni “free style”.
Kulingana na Dizo, siri ya kufanikiwa ni kujitolea na kujihini pamoja na kujiamini. Unapoanza jambo, usitazame nyuma hata kidogo au hata kujishuku. Mungu akiwa nawe kila kitu hufanikiwa katika wakati wake.
“Siwezi kurudi nyuma kamwe. Nalenga kujiunga na kundi la WCB Wasafi siku moja. Nikipata mfadhili anayeweza kunisaidi katika kujenga kariha yangu nitafurahi sana,” alisema mgeni wetu kwa matumaini makuu.