Ruto awasuta wanaotaka ajiuzulu
Na SAMMY WAWERU
NAIBU Rais William Ruto amewasuta vikali wapinzani wake kwa kumtaka ajiuzulu kufuatia hatua yake kuikosoa mara kwa mara serikali aliyomo.
Dkt Ruto amesema aliye na mamlaka kumuondoa usukani, ni wananchi waliomchagua pamoja na Rais Uhuru Kenyatta.
Licha ya baadhi ya wapinzani wake kushinikiza ajiuzulu kwa kile wanadai “haiwezekani kuikosoa serikali unayoongoza ilhali unataka kuhusishwa na maendeleo yake”, naibu rais alisema hatakubali kupewa presha na yeyote ang’atuke.
“Nilichaguliwa na Wakenya waliomchagua Uhuru Kenyatta, wao ndio wataamua iwapo ninapaswa kuwa madarakani au la,” Dkt Ruto akasema.
Wandani wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga wamekuwa wakimkosoa naibu rais kufuatia malalamishi yake kuwa anahujumiwa hasa baada ya mapatano kati ya Rais Kenyatta na Bw Raila, maarufu kama Handisheki.
Rais na Waziri huyo Mkuu wa zamani walitangaza kuzika tofauti zao za kisiasa Machi 2018, salamu za maridhiano ambazo zimeonekana kumpa Raila mamlaka kushiriki katika maamuzi muhimu ya serikali.
Aidha, Dkt Ruto analalamikia kutengwa katika serikali anayohoji “niliiunda na Rais Kenyatta”.
Vilevile, anateta kupokonywa majukumu yake kama naibu wa rais, yakipokezwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Alfred Matiang’i.
“Wewe ni nani kuniambia nitoke? Walionichagua niwafanyie kazi hawajaniambia,” Ruto akachemka.
Alitoa matamshi hayo Jumatatu jioni, katika mahojiano na Weru TV, runinga inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kimeru.
Uhusiano wa Rais Kenyatta na naibu wake unaendelea kudorora, kiasi cha viongozi hawa kurushiana cheche za maneno hadharani.
Katika hafla kadha za umma, kiongozi wa nchi amenukuliwa akimjibu Dkt Ruto “ikiwa amechoka na serikali mlango u wazi aondoke”.
Kambi ya Ruto, chini ya chama cha UDA na ambacho ametangaza kuwania urais nacho 2022, imekuwa ikilalamikia hatua ya baadhi ya mawaziri kujihusisha na siasa, na kudai kumdunisha naibu rais.
Naibu rais anasema endapo atamrithi Rais Kenyatta mwaka 2022, ataendeleza miradi waliyoanza chini ya serikali ya Jubilee.
Ruto aidha amekuwa akijihusisha na wananchi wa mapato ya chini, chini ya vuguvugu la Hasla akitoa mamilioni ya pesa kuinua biashara za vijana, kina mama mboga na wahudumu wa bodaboda.
Wapinzani wake wamekuwa wakikosoa kiini cha fedha zake, wakitaka apigwe msasa na kumhusisha na sakata za ufisadi.
Next article
Kukubo angali na ndoto ya kuwa rais wa Kenya