Connect with us

General News

Ruto, Raila wakosa kipya cha kuahidi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Ruto, Raila wakosa kipya cha kuahidi – Taifa Leo

Ruto, Raila wakosa kipya cha kuahidi

Na BENSON MATHEKA

WAGOMBEAJI wakuu wa urais kwenye uchaguzi mkuu ujao wanaonekana kuishiwa na ajenda na sera za kuuzia Wakenya na sasa wamebaki kupakana matope.

Japo mikutano wanayofanya maeneo tofauti nchini imekuwa ikivutia watu wengi wanaowasikiliza, Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanaonekana kukosa kipya za kuwaelezea wapigakura.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Derrick Aswani, japo wanasiasa kupakana matope wakati wa kampeni sio jambo geni Kenya, inaonekana wagombeaji wakuu wa urais kwenye uchaguzi ujao wameingiwa na uchovu wa kimawazo.

“Baadhi yao wamekuwa kwenye kampeni kwa miaka minne na hawana kipya cha kuwaambia wapigakura isipokuwa kubomoa wapinzani wao. Hali hii itaendelea uchaguzi mkuu unapokaribia,” asema Bw Aswani.

Dkt Ruto anavumisha muungano wa Kenya Kwanza Alliance (KKA) unaoleta pamoja chama chake cha United Democratic Alliance UDA, Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi na Ford Kenya cha seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula kwa kumshambulia Bw Odinga kibinafsi.

Naye Bw Odinga anatumia vuguvugu lake la Azimio la Umoja akiungwa mkono na chama tawala cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta na vyama vingine vidogo kumpaka matope Dkt Ruto na washirika wake katika KKA.

KUCHAFULIANA SIFA

Badala ya kufafanulia wapigakura atakavyotekeleza mfumo wake wa kufufua uchumi ambao amekuwa akivumisha kwa miaka minne iliyopita, Dkt Ruto amekuwa akimtaja Bw Odinga kama tapeli na mzee wa vitendawili ambaye hana kipya kwa Wakenya.

“Raila anapenda uongo na utapeli wa kisiasa. Ikiwa mtu ni tapeli wa kisiasa hata hawezi kuaminiwa na viongozi wenzake ndiposa wanatuunga mkono ili kumkomesha,” Dkt Ruto alisema akiwa Limuru, Kaunti ya Kiambu mnamo Jumapili.

Ilikuwa mara yake ya tatu kwa Dkt Ruto kurudia kauli hilo katika kipindi cha siku tatu. Akiwa katika kaunti za Kirinyaga na Embu wikendi iliyopita, Naibu Rais aliongoza washirika wake kumshambulia Bw Odinga wakimtaja kama kiongozi aliyezoea kusaliti na kuhadaa viongozi na wafuasi wake.

Kwa upande wake, badala ya kueleza wapigakura atakavyoleta umoja nchini, Bw Odinga na viongozi wanaomuunga mkono katika vuguvugu la Azimio la Umoja wamekuwa wakimrushia mishale Dkt Ruto na washirika wake wapya, Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula wakidai ni wezi, wazembe na wasioweza kuaminika.

“Nimefanya kazi na watatu hao na niliwapa kazi lakini wakabadilika kuwa wezi. Nilimfuta kazi mmoja wao lakini akaokolewa na Kibaki. Hawa ndio sasa watu wanataka kukomboa Kenya? Waende nyumbani!” Bw Odinga alisema Jumapili akiwa mtaani Kawangware.

Ni kauli aliyotoa kwanza akiwa katika mkutano wa siasa katika uwanja wa Ihura, Kaunti ya Murang’a siku iliyotangulia.

MADAI

“Inasemwa kwamba watu wa tabia sawa hujumuika pamoja na sasa mnavyoona wameungana. Hawa ndio watu mnaotaka kuchagua na mtarajie wawaletee maendeleo? Makao yao yanafaa kuwa Kamiti,” Bw Odinga alisema.

“Wanaiba pesa kisha wanarudi nazo kwa magunia na kuzitumia kutoa hongo na michango katika harambee,” alisema Bw Odinga.

Seneta wa Siaya James Orengo ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga alitaja mfumo wa uchumi wa Dkt Ruto wa kusaidia maskini kujiinua kiuchumi kama ujinga.

“Unaambia watu utawatoa kutoka umaskini ilhali ni wewe uliwaweka huku chini. Hatutaki ujinga kama huo,” Bw Orengo alisema akiandamana na Bw Odinga kwenye kampeni mtaani Kawangware.