CHARLES WASONGA: Uhuru, Ruto wadumishe amani nchini kipindi hiki cha kampeni
Na CHARLES WASONGA
KWA mujibu wa Katiba ya sasa asasi ya Urais inajumuisha afisi ya rais na afisi ya naibu rais.
Urais unawakilisha umoja, uthabiti na maendeleo ya taifa la Kenya. Asasi hii wakati huu inasimamiwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, ambao ndio viongozi wenye ushawishi mkubwa nchini na serikalini.
Wawili hawa wameshikanishwa na katiba tangu wanapoomba kura hadi kipindi chao cha kuhudumu kitakapokamilika. Kwa hivyo, licha ya tofauti ambazo zinaweza kutokea baina yao, sharti wasalie pamoja.
Kimsingi, tofauti na Katiba ya zamani, Rais Kenyatta hawezi kumfuta kazi Dkt Ruto japo aelewani naye kisiasa ilivyo sasa.
Licha ya wawili hawa kutofautiana kuhusiana na siasa za urithi wa Urais, kipengele cha 147 (3) cha Katiba kinampa Dkt Ruto idhini ya kuwa kaimu rais endapo hali itatokea ambapo Rais hataweza kutekeleza majukumu ya afisi yake.
Kwa mfano, mnamo Oktoba 7, 2014 Rais Kenyatta alimteua Dkt Ruto kama Rais wa muda alipojiwasilisha katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) kujitete kuhusiana na kesi iliyohusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.
Licha ya kudai kuwa ametengwa, serikalini Dkt Ruto bado anaendelea kufurahia hadhi na ushawishi wa afisi hiyo kando na kuendelea kutumia mali ya umma. Kwa mfano, inakadiriwa kuwa ziara yake ya siku 10 nchini Amerika, Uingereza na Qatar imemgharimu Mkenya mlipa ushuru karibu Sh107 milioni.
Kando na hayo, Dkt Ruto alipokewa na balozi wa Kenya nchini Amerika Lazarus Amayo. Aidha, serikali ya Amerika ilimpa Dkt Ruto walinzi na magari aliyotumia katika shughuli zake nchini, hadhi inayostahiki afisi anayoshikilia katika serikali ya Kenya. Kwa hivyo, ilikuwa Dkt Ruto hakufaa kuishambulia serikali hii anayoitumikia kama Naibu Rais.
Isitoshe, kama mwanachama wa baraza la mawaziri na Kamati ya Usalama Nchini (NSC) Dkt Ruto ni sehemu ya maafisa wa serikali waliotwikwa mamlaka ya kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao unaendeshwa katika mazingira huru na haki.
Dkt Ruto ni miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali wenye wajibu wa kuhakikisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inasaidiwa ili iweze kutekeleza wajibu wake wa kusimamia na kuendesha uchaguzi mkuu ujao kwa njia huru na haki.
Hafai kulalamika kuwa serikali, ambayo anaitumikia, inapanga kuiba kura za urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Aidha, haina maana kwa Dkt Ruto kuwaomba jamii ya kimataifa iingilie shughuli hiyo ili kuzuia kutokea kwa uovu huo.
Matamshi kama hayo ni hatari kwa sababu yanaonyesha kuwa IEBC haitaweza kusimamia uchaguzi huo kwa njia huru inavyotarajiwa. Yanaashiria kuwa Dkt Ruto amekosa imani na tume hii ambayo kwa mujibu wa Katiba, haipaswi kuingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa hivyo, Naibu Rais kama mmoja wa wawaniaji urais wakuu anawapa wafuasi wake sababu ya kukataa matokeo ya uchaguzi wa urais endapo mtu mwingine atatangazwa kuwa mshindi.
Hii ni hatari kwa usalama wa taifa hili kwa sababu ghasia zinaweza kutokea nchini ilivyofanyika baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo jumla ya watu 1,500 waliuawa na wengine 650, 000 wakafurushwa makwao.
Dkt Ruto akome kabisa kutoa matamshi ambayo yanaweza kusababisha vita nchini. Kama mshikilizi wa afisi ya naibu rais, ana wajibu wa kushirikiana na Rais Kenyatta katika kudumisha amani na utulivu nchini kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.