UhuRuto walivyofuta mafanikio ya Kibaki
NA PETER MBURU
KUFIKIA Machi 2013 alipomaliza miaka 10 uongozini, mwendazake rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki aliacha taifa katika mwelekeo mzuri kiuchumi.
Hii ni baada yake kukuza utajiri wa taifa (GDP) kwa asilimia 367 tangu alipoingia madarakani mnamo 2002 na kulikomboa kutoka shimo la madeni.
Alipoingia uongozini 2002, Mzee Kibaki alipokea Kenya iliyokuwa na utajiri wa Sh1 trilioni kutoka kwa mtangulizi wake Daniel Moi.
Hata hivyo, mabadiliko aliyoleta ya kiuchumi kama vile kuwekeza katika sekta za elimu, afya na kufadhili wananchi kupata mikopo kwa riba ya chini ili kufanya biashara, yaliinua uchumi wa Kenya na kuboresha maisha ya wananchi kwa viwango ambavyo havikuwahi kushuhudiwa awali.
Alipokuwa akiondoka 2013, deni la Kenya lilikuwa asilimia 46.5 ya utajiri wa kitaifa kutokana na kukua kwa uchumi na kukopa madeni ya riba ya chini na masharti nafuu ya kulipa, hali iliyokomboa Kenya kutoka masharti ya waliokuwa wakiikopesha kuhusu jinsi ya kuendesha shughuli zake.
Sarafu ya Kenya pia ilikuwa imeimarika kwa kiwango kikubwa na hivyo kupunguzia serikali mzigo wa madeni.
Hata hivyo, miaka 10 ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto imefuta mengi ya mafanikio aliyokuwa amepiga marehemu Kibaki.
Kiwango cha deni la taifa kimepanda hadi Sh8.02 trilioni kufikia Desemba 2021, ama asilimia 66.2 ya utajiri wa taifa, na hivyo kurudisha Kenya katika shimo la madeni ilimokuwa kabla ya Rais Kibaki kuingia uongozini.
Kiwango kinachotumika kulipa madeni kimepanda kwa zaidi ya asilimia 500, huku Afisi ya Masuala ya Bajeti Bungeni (PBO) ikikadiria kuwa serikali itatumia Sh1.36 trilioni kulipa madeni mwaka 2022/23, mzigo mkubwa ukiwa kulipia riba ya mikopo hiyo.
Chini ya uongozi wa Mzee Kibaki, Serikali ilikuwa imepunguza ukopaji kutoka kwa benki za kibiashara nchini, hali ambayo ilihakikisha benki hizo zina pesa za ziada za kukopesha wananchi wa kawaida kwa riba ya chini.
IMF, BENKI YA DUNIA ZIMERUDI
Lakini uongozi wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto ulizima mwanya huo uliosaidia wananchi wengi kujiinua kibiashara kwa kukopa kupindukia kutoka kwa benki hizo.
Madeni kutoka benki hizo za kibiashara yamepanda kwa kiwango kikubwa zaidi cha asilimia 1,957.
Kutokana na kuwa benki hizo zinakopesha serikali kwa riba ya juu na muda mfupi wa kulipa, nyingi zinaamua kuikopesha kuliko wananchi.
“Jumla ya Sh17.47 bilioni zilitumika kulipa madeni ya nje Desemba 2021, zikihusisha Sh8 bilioni kwa malipo ya madeni yenyewe na Sh9.47 bilioni kulipia riba. Malipo kwa mataifa mengine yalijumuisha asilimia 28.7 huku kwa benki za kibiashara yakijumuisha asilimia 53 na mashirika ya kimataifa asilimia 18.3,” Wizara ya Fedha ikasema katika ripoti ya punde zaidi kuhusu madeni.
Katika utawala wake, marehemu Kibaki alifanikiwa kupunguza ushawishi wa mashirika ya IMF na Benki ya Dunia katika masuala ya nchi.
Lakini miaka 10 tangu alipostaafu, IMF na Benki ya Dunia yamerudi kwa fujo na sasa ndiyo yanayoelekeza serikali kuhusu jinsi inavyoendesha uchumi na masuala ya kijamii.
Akihutubia taifa majuzi kuhusu Bajeti ya 2022/23, Waziri wa Fedha Ukur Yatani alizungumzia vikubwa jinsi serikali inatii masharti ya IMF, kama vile kusukuma mashirika kupunguza idadi ya wafanyakazi na kupunguzia ufadhili wa sekta zenye manufaa kwa jamii.
Sarafu ya Kenya (Ksh) ambayo ilikuwa imeimarika chini ya Rais Kibaki hadi kupunguza mzigo wa kulipa madeni na kuagiza bidhaa kutoka nje sasa imezorota, hivi kwamba dola ya Marekani inabadilishwa kwa zaidi ya Sh115 za Kenya.
Rais Kibaki alikuwa ameboresha sarafu ya Kenya dhidi ya dola ya Marekani kutoka ubadilishanaji wa Sh77.3 alipoingia 2002, ikashuka hadi Sh63.7 kufikia 2007 na alipoondoka ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh85.64.
UMASKINI UMEONGEZEKA
Kuzorota kwa sarafu ya Kenya kunamaanisha kuwa wafanyabiashara wanapoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi wanatumia pesa nyingi kuzilipia na hivyo bei yake nchini inapanda, na pia serikali inatumia pesa nyingi kulipa madeni ambayo yanalipwa kwa sarafu za mataifa mengine.
Umaskini pia umepanda chini ya utawala wa UhuRuto, ambapo ripoti ya majuzi ya ya Taasisi ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera za Umma (Kippra) inaeleza kuwa Wakenya milioni 16 wametumbukia katika umaskini tangu Rais Kenyatta na Dkt Ruto hao walipochukua madaraka.
Kiwango hicho cha umaskini kimepanda kufikia asilimia 63 ya taifa, kutoka asilimia 38.9 ya taifa mnamo 2014, mwaka mmoja tu baada ya serikali ya UhuRuto kuingia uongozini.