Hakimu asimulia jinsi alivyoponea kifo wakati wa shambulio la al-Shabaab
NA STEPHEN ODUOR
JUMATANO, Januari 26, 2022 itasalia siku atakayokumbuka Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Garsen Paul Rotich.
Anasema ni siku atakayoikumbuka licha ya kwamba lilikuwa tukio la kuogofya ili akumbuke neema ya Mungu juu ya maisha yake.
Bw Rotich alikuwa miongoni mwa maafisa watano wa Mahakama ya Garsen ambao walishambuliwa katika eneo la Lango La Simba na washukiwa wa al-Shabaab.
Walikuwa wametoka katika kikao cha mahakama katika kijiji cha Kipini, Kaunti ya Tana River walipovamiwa na watu waliokuwa wamejihami.
“Tulikuwa tunazungumza tu jinsi siku hiyo ilivyokuwa na mafanikio. Mbele yetu kulikuwa na lori na ghafla genge lenye silaha kutoka msituni lilijaribu kutusimamisha,” akasimulia.
Mwanzo anasema yeye na maafisa wengine wa mahakama walifikiri kuwa kundi hilo lilikuwa kikosi cha usalama kinachopiga doria katika barabara hiyo. Lakini walipokaribia kusimama pale, afisa wa usalama aliyekuwa nao alitambua upesi kwamba bunduki zao hazikuwa rasmi na kumtaka dereva aongeze kasi.
“Walipoona dereva wetu anaongeza kasi, walirusha gruneti ambalo lililikosa gari, kisha kufyatua risasi iliyoshika usukani wetu na kioo cha mbele, dereva akafia barabarani,” alisimulia.
Gari hilo liliposimama walijua kuwa wamefika mwisho. Baadhi yao walikuwa wamepigwa risasi, lakini wakapata ujasiri na kuliacha gari hilo kukimbia kuokoa maisha yao.
Tukio hilo lilikuwa likitokea karibu na kambi ya kijeshi katika maeneo hayo.
“Nilikuwa katika hali ya hofu lakini nakumbuka mwendesha mashtaka alinitoa nje na kunitaka nisonge nami nikajisemea, risasi ikinikuta basi inikute kutokea nyuma,” alisema.
Mguu niponye
Walisahau majeraha yao na kukimbilia porini huku kila mmoja akitafuta pa kujificha kutokana na risasi zilizokuwa zikinyesha kutoka kwa washambuliaji wao.
Wakati huo huo, washambuliaji walikuwa wakielekea kwenye gari.
Muda mfupi baadaye, wanajeshi walijibu tukio hilo, na vikundi hivyo viwili vilirushiana risasi na kurushiana gruneti.
Washambuliaji waliacha makabiliano na kuanza kurudi walikotoka. Hata hivyo, walichukua sanduku la stakabadhi za mahakama na funguo la gari lile.
“Bunduki ziliponyamaza, askari wa jeshi walifika porini na kutuita nje, wote tulikuwa tunasubiri kifo wakati huo, tulikuwa tumekata tamaa, tulipuuza wito wa kwanza hadi yule askari alipozungumza Kiswahili na kujitambulisha,” alisimulia.
Zilikuwa ni dakika 20 za kutisha ambazo maafisa hao wataishi kukumbuka.
Kulingana na Bw Rotich, mwendesha mashtaka aliponea kupigwa risasi kichwani na ana alama kwenye sehemu yake ya juu kidogo ya paji la uso lililopondwa na risasi.
Hakimu huyo anabainisha kuwa hakutarajia tukio kama hilo kwani hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kufika Kipini kwa majukumu ya mahakama katika juhudi za kuimarisha upatikanaji wa haki.
Sasa tukio hilo linamwacha na maswali chungu nzima.
Je, alisalitiwa na watu wale wale alioenda kuwatolea huduma au alikuwa ni mwathiriwa wa hali mbaya tu?
Kinachomhuzunisha zaidi ni kwamba watu wa Kipini huenda wakarejea katika mahangaiko ya hapo awali ambapo walilazimika kusafiri makumi ya kilomita hadi mahakama ya Garsen ili kesi zao zishughulikiwe.
“Tulikuwa tumepiga hatua katika upatikanaji wa haki. Kilichotokea kinaweza kudhibitiwa kwa kuweka ulinzi mkali kwenye barabara hiyo,ili kuhakikisha watu wangu wa Kipini hawarudi kwenye mateso,” anasema.
Meneja wa mradi wa Upatikanaji wa Haki – Access to Justice – Stephen Otoi alitaja kisa hicho dhidi ya maafisa wa mahakama kuwa cha kusikitisha, hivyo basi kusisitiza haja ya kuwa na ulinzi mkali kwa maafisa wa mahakama katika Kaunti ya Tana River.
“Kaunti hii ni pana na ina pembezo, kila mtu hawezi kufika kortini. Kwa hivyo, haja ya kuwa na mahakama kukutana nao wakati wa mahitaji yao, Wizara ya Usalama wa Ndani inapaswa kuchukua suala hili kwa uzito mkubwa,” alisema.
Bw Otoi anabainisha kuwa maafisa wa serikali katika kaunti ya Lamu na Tana River wanapaswa kugawiwa, maafisa wa usalama na kusindikizwa katika juhudi za kutekeleza majukumu yao.