Hisia mseto Wakenya wakiambiwa sasa barakoa si lazima
NA MWANGI MUIRURI
HATUA ya Waziri wa Afya Bw Mutahi Kagwe, Ijumaa ya kuondoa ulazima wa kuvaa barakoa imetajwa na wengi kama mwisho wa utumwa.
Wakenya wengi wamesema kuwa sasa watapumua ikizingatiwa kuwa kwa wakati mrefu barakoa ilikuwa mavuno kwa polisi.
“Tangu barakoa iingie katika maisha ya Wakenya kwa msingi wa kuzuia usambazaji wa virusi vya corona, wengi wamejipata katika sakata ya kukamatwa na kisha kushurutishwa kulipa hongo ya kati ya Sh2,000 na Sh10,000 ili kuachiliwa huru,” asema Mwenyekiti wa Madiwani eneo la Mlima Kenya Bw Charles Mwangi.
Bw Mwangi aliye pia diwani wa Ichagaki katika Kaunti ya Murang’a alisema kwamba sasa Wakenya wako na uhuru wa kukoma ule unafiki wa kuvaa barakoa kwa minajili ya kuhepa kukamatwa wala sio wa kujikinga maradhi.
“Kuna maafisa wa polisi ambao wameomboleza kufungwa kwa ‘shamba la mavuno bila jasho’ ambapo wengi wao wamevuna donge nono haramu kupitia kuuza uhuru kwa waliokamatwa bila barakosa,” akasema.
Wakili Timothy Kariuki wa mahakama Kuu anasema kwamba “barakoa ilikuwa sio sheria bali ilikuwa tu ni ilani ya Wizara ya Afya.”
Anasema kwamba sheria ya kutumika kuhukumu watu katika mahakama huwa ni ile imejadiliwa katika bunge la kitaifa kwa ushirikiano wa seneti na kuidhinishwa na Rais.
“Lakini wakati janga la Covid-19 lilipoingia maishani mwetu na kila mdau akawa amechanganyikiwa na maoni ya kujikinga yakaanza kutolewa, ndipo ilisemwa kwamba kumewekwa sheria ya barakoa,” asema Bw Kariuki.
Agizo hilo la wizara kuwa watu wawe wakijipamba barakoa kwa pua na mdomo iliandamanishwa na adhabu ya Sh20,000 au kifungo cha miezi sita gerezani, au adhabu zote mbili.
Maafisa wa polisi walizindua kilio nchini baada ya kugeuza barakoa kuwa kiini cha misako na kudai mlungula.
Akiondoa ilani hiyo, Bw Kagwe alisema kwamba maambukizi ya corona nchini yako katika kiwango cha asilimia moja.
“Katika hali hiyo ambayo sasa imedumu kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, hakuna ile dharura ya kuvaa barakoa,” akasema.
Seneta wa Murang’a Dkt Irungu Kang’ata alisema kuwa hakuna geni ambalo Bw Kagwe amesema kwa kuwa hata wengi wa polisi, mawaziri na wanasiasa hawakuwa wakiivaa.
“Mikutanoni, mitaani, ofisini… watu walikuwa hawaizingatii barakoa na kile tu Bw Kagwe amefanya ni kutuondolea usumbufu wa kudaiwa hongo na polisi,” akasema.
Dkt Kang’ata alisema kwamba usumbufu uliokuweko utaanza kujidhihirisha mara moja kupitia Wakenya wengi kuitupilia mbali mara moja.
“Hata waliokuwa wakiivaa walikuwa wanaiweka kwa mashavu, wengine kwa mfuko na kuivaa wakiona maafisa wa polisi. Hata tulikuwa tukishuhudia upumbavu wa maafisa wasio na barakoa wakiwakamata raia kwa kutoivalia,” akasema Bw Kang’ata.
Lakini mchuuzi wa barakoa mjini Murang’a Bi Cecilia Wamaitha anasema kuwa amepoteza riziki.
“Nitaishi kukumbuka jinsi uchuuzi wa barakoa ulivyonisaidia kupata lishe. Kufikia mwezi wa sita 2020, barakoa moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh50. Lakini kufikia wakati Bw Kagwe aliitupilia mbali, ilikuwa ikiuzwa hata kwa Sh3,” akasema.
Hali ilivyo mtaani Maragua katika Kaunti ya Murang’a Machi 11, 2022, raia wakishiriki shughuli za sokoni ambapo wengi hawajavalia barakoa. PICHA | MWANGI MUIRURI
Alisema kwamba wakati ilikuwa ikiuzwa kwa Sh50, faida ilikuwa Sh45.
“Ni kweli kila kilicho na mwanzo huwa kina mwisho. Kwaheri faida kwangu na kwaheri ya hongo kwa maafisa wa polisi. Ni utumwa wa barakoa umefika kikomo pia,” akasema.
Bw Kagwe alisema kwamba kwa sasa kuvaa barakoa au kutoivaa ni maamuzi ya kibinafsi na hakuna kuwindwa na maafisa wa usalama sasa kwa kuikosa mdomoni.