Connect with us

General News

KPA yashtakiwa kuhusu zabuni ya ujenzi bandari – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

KPA yashtakiwa kuhusu zabuni ya ujenzi bandari – Taifa Leo

KPA yashtakiwa kuhusu zabuni ya ujenzi bandari

NA PHILIP MUYANGA

MWANAHARAKATI Okiya Omtatah ameishtaki halmashauri ya Bandari nchini (KPA) kwa kutoa zabuni ya ujenzi wa bandari ya samaki iliyopendekezwa eneo la Shimoni, Kaunti ya Kwale awamu ya kwanza kwa kampuni ya Southern Engineering (Seco).

Bw Omtatah anasema kuwa kuna mgongano wa kimaslahi kwa kuwa Seco ndio walikuwa washauri wa mradi huo na hivyo basi kutayarisha stakabadhi za zabuni na pia kuhusika katika zabuni hiyo na kushinda.

Mwanaharakati huyo anasema kuwa, KPA ilikuwa imewasilisha kampuni nane kutoa zabuni kwa ujenzi wa bandari hiyo awamu ya kwanza kabla ya kuwapatia stakabadhi za zabuni hiyo.

Zabuni hiyo, Bw Omatatah anasema kuwa ilifunguliwa Disemba mwaka jana na Machi 24 KPA ikatangaza kuwa imeipa Seco zabuni hiyo.

Kulingana na mwanaharakati huyo,Seco haikuwa imewasilisha kiwango cha chini katika zabuni hiyo kwani ilisema itagharimu Sh2.6 bilioni ambayo ni juu ya kiwango cha Sh1.7 bilioni kilichotengewa mradi huo katika bajeti ya KPA.

Katika kesi yake aliyoiwasilisha katika mahakama kuu mjini Mombasa,Bw Omtatah anasema kuwa kupeanwa kwa zabuni hiyo kwa Seco hakuwezikani kwa kuwa kunazua mgongano wa maslahi kwa kuwa kampuni hiyo ni mshauri na mkandarasi kwa mradi huo mmoja.

Mwanaharakati huyo anataka mahakama kuamua ya kuwa,kwa kuwa mshauri aliyeshughulika na kutengeneza stakabadhi za zabuni, Seco ilikuwa haiwezi kushiriki katika zabuni hiyo ya ujenzi wa bandari ya samaki uliopendekezwa awamu ya kwanza.

Pia anataka agizo litolewe la kufutilia mbali kupeanwa kwa zabuni na KPA kwa kampuni hiyo ya uhandisi ya Seco.

Bw Omtatah pia anasema kuwa kukubali mshauri wa mradi huo kupewa zabuni ya ujenzi ni ubaguzi na pia ni kupigana dhidi ya haki za uchumi na kisosholojia za wanakandarasi wengine.

“Mwasilishaji kesi anashuku kuwa Seco imependelewa kinyume cha katiba ili kutimiza malengo ambayo hayafai au kuendeleza maswala ya ufisadi,” alisema Bw Omtatah.

Aliongeza kusema kuwa kula njama,mgongano wa kimaslahi,na ghiliba kuhusiana na kupeanwa kwa zabuni hiyo kunaweka chini ushindani wa haki na thamani ya pesa kinyume cha sheria.