JIJUE DADA: Kuzuia ngozi kuzeeka mapema
Na PAULINE ONGAJI
MOJAWAPO ya changamoto kuu zinazowakumba wanawake ni tatizo la ngozi kuzeeka mapema.
Kuna mambo mengi yanayosababisha shida hii lakini mbinu hizi zitakusaidia kukabili hali hiyo:
· Lishe bora: Hii ndio siri ya afya bora katika sehemu zote mwilini. Mboga na matunda husaidia kuunda upya ngozi iliyoharibika. Na kwa upande mwingine, chakula kilicho na viwango vya juu vya kabohaidreti na mafuta huchochea kuzeeka. Pia, kunywa maji kwa wingi kutakusaidia kuimarisha ubora wa ngozi yako.
· Jua: Kila wakati hakikisha unalinda ngozi yako kutokana na miyale ya jua. Jizoeshe kukaa kwenye kivuli, kujifunika, kuvalia kofia na miwani ya jua na hata kujipaka sunscreen ukitembea kwenye jua.
· Mazoezi: Kiwango wastani cha mazoezi chaweza kuongeza mzunguko wa damu mwilini. Hii huimarisha mfumo wa kingamwili na hivyo kuifanya ngozi yako kuonekana changa.
· Usafi: Hakikisha kwamba unaondoa vipodozi usoni kabla ya kulala usiku. Aidha, nawa uso wako mara mbili kwa siku: Hii itasadia kuondoa jasho ambalo husababisha mwasho. Unapofanya hivi hata hivyo, usisugue ngozi yako kwa nguvu.
Baada ya usafi, paka mafuta kila siku ili kuzuia maji yasipenyeze na kutoka kwenye ngozi.
· Ishara za uso: Unapofanya ishara kwa uso kama vile kufanya makengeza, unabana misuli iliyoko chini ya ngozi. Na ikiwa utabana misuli hii kwa miaka mingi, mistari hii inakuwa ya kudumu. Kuvalia miwani ya jua husaidia pia kupunguza tatizo hili.
· Epuka sigara, pombe na bidhaa za ngozi zinazosababisha mwasho kwenye ngozi.
Uvutaji sigara huongeza uwezekano wa ngozi kuzeeka kwani mbali na kusababisha makunyato, hufanya ngozi yako kunyauka. Kwa upande mwingine, pombe hukausha unyevu kwenye ngozi na baada ya muda kusababisha uharibifu.
Hii yaweza kukufanya uonekane mzee. Bidhaa za ngozi zinazosababisha mwasho, nazo huchoma sehemu hii. Hii yaweza sababisaha ngozi yako kuonekana kuzeeka.
Next article
Smalling aongoza AS Roma kutandika Spezia katika Serie A