Connect with us

General News

Mitandao ya ukora Kirinyaga – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mitandao ya ukora Kirinyaga – Taifa Leo

MAKALA MAALUM: Mitandao ya ukora Kirinyaga

NA MWANGI MUIRURI

KINAYA cha Kaunti ya Kirinyaga ambayo ni nyumbani kwa Katibu maalum wa Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho kuathirika na mitandao ya ujambazi kinazidi kujiangazia katika maisha ya wenyeji.

Huku Dkt Kibicho akiwa ni hasidi sugu wa ulevi kiholela na biashara ya mihadarati na ambapo amekuwa akionekana nyanjani akiwafuta kazi maafisa wa usalama waliozembea katika kupambana na hali hizo, hali sasa inaonekana kumwendea kinyume katika Kaunti yake ya kuzaliwa ambapo kwake nyumbani ni katika mji wa Kagio.

“Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia visa vya raia sambamba na maafisa wa kudumisha usalama wakishiriki visa vya uhalifu. Kwa sasa, kuna maafisa watano wa polisi ambao wako na kesi kortini ambapo wamedaiwa kumwibia mfanyabiashara mmoja Sh80, 000 kwa kutumia mabavu. Ni kisa kilichofanyika Desemba 5, 2021 ambapo mfanyabiashara huyo wa kiume alilalamika kuwa alitekwa nyara na maafisa hao, akaingizwa katika gari rasmi la polisi na hatimaye akawasilishwa hadi kwa mtambo wa kutoa pesa za benki (ATM) na akaagizwa awatolee kitita hicho,” asema mwenyekiti wa haki za wafanyabiashara katika Kaunti hiyo Simon Muriithi.

Bw Muriithi anasema kuwa mitandao ya wauzaji pombe kwa masaa ya kinyume na sheria, walanguzi wa mihadarati na pia wawekezaji wa mitambo ya uchezaji Kamari imeenea katika Kaunti zote ndogo tano za Kirinyaga. Kaunti hizo ni Kirinyaga Mashariki, Magharibi, Kati, Mwea Mashariki na magharibi.

“Dkt Kibicho amekuwa akisisitiza kwamba ni lazima kaunti yake ya nyumbani iwe kielelezo bora katika kutii sheria na kudumisha amani ndio akiwarai wengine kitaifa wawe wakenya wema, awe na mashiko ya kuwa mfano mwema. Lakini kwa sasa Kaunti hii yetu inamuaibisha,” akasema.

Mbunge wa Mwea Bw Kavinga wa Thayu alikiri kwamba matukio ya Kaunti hiyo katika siku za hivi majuzi yanaonyesha waziwazi kwamba wadau wanafaa wamakinikie suala la usalama wa Kirinyaga.

“Tumeshuhudia ukora wa kila aina miongoni mwa wahudumu wa bodaboda. Tumeona magenge ya vijana ambayo yamechipuka kwa misingi ya kisiasa. Baa zetu hazina utaratibu na pombe inauzwa kiholela huku vijana kwa wazee wakizama kwa mtindi kiasi kwamba umasikini unawafuata,” akasema.

Ni Kaunti ambayo imesajili ongezeko kubwa la vijana wa kurandaranda mitaani na ambao huonekana katika steji na vichochoro wakilewa na kususia shule licha ya kuwa ni sheria nchini kila mtoto ashiriki kwa ulazima elimu hadi ya Sekondari.

Aidha, ni Kaunti ambayo miji yake mingi imejaa wasichana wa umri mdogo wakishiriki biashara ya ukahaba, ajira ya watoto na visa vya wazazi walevi kufika katika magweni na mabaa wakibeba watoto wachanga.

Gavana wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru aliteta kuwa vyombo vya usalama vimeelekezwa kwa siasa na ndio sababu visa vya utovu wa kiusalama vinaendelea kuchipuka.

“Sisi katika siasa na huduma kwa watu wa Kirinyaga kupitia serikali yetu ya ugatuzi tunapoendelea na kuchapa kazi, navyo vyombo vya usalama vimeelekezwa kucheza siasa. Kwa kuwa sisi wengi ndani ya Kaunti tuko katika mrengo wa United Democratic Alliance (UDA) huku naye Dkt Kibicho akiwa wa Azimio la Umoja, ametelekeza majukumu yake ya kutulinda akifuatana na siasa,” akasema.

Bi Waiguru aliteta kuwa “badala ya Dkt Kibicho asukumane na kuimarisha usalama na maendeleo ya Kirinyaga kama mwenyeji, kazi yake imekuwa ya kutupiga vita vya kisiasa na kutumia vitengo vya kiusalama kuingilia mikondo ya siasa.”

Kaunti ya Kirinyaga ambayo ina upana wa Kilomita 1,478 mraba husifika na kilimo cha mpunga ambapo huzaliosha asilimia 80 ya mchele wote ambao huliwa hapa nchini.

Sifa nyingine ya Kaunti hii ni kuwa ni miongoni mwa zile tatu ambazo mwaka wa 2017 zilichagua magavana wa kike, Bi Anne Waiguru akichaguliwa sambamba na Bi Charity Ngilu wa Kitui na marehemu Joyce Laboso wa Bomet.

Ni Kaunti ambayo ni nyumbani kwa mwenyekiti wa Narc Kenya, Bi Martha Karua na ambaye kwa sasa amejiunga na mrengo wa Azimio la Umoja na anasemwa kuwa na uwezekano wa kuteuliwa kuwa mgombezi mwenza wa Bw Raila Odinga anayewania urais. Katika uchaguzi wa 2017, Bi Karua aliangushwa katika kura ya ugavana na Bi Waiguru. Pia, Bi Karua alikuwa amewania urais 2013 na ambapo alizoa kura 43, 000 kote nchini.

Kamanda wa Polisi wa Kirinyaga Bw Mathews Mang’ira aliambia Taifa Leo kwamba hakuna suala lolote ambalo limeenda mrama kiusalama.

“Usiwe na shaka kwamba kuna lolote ambalo limetulemea. Tunapambana na hali yetu. Kwa sasa tumezindua misako dhidi ya mitandao yote ya ukora na jata katika majukwaa ya siasa, tumezidisha doria za kuzima ghasia,” akasema.

Alisema kuwa kile kinachohitajika ni wananchi washirikiane na maafisa wa kiusalama kupitia kuwapasha habari muhimu kuhusu majambazi na habari muhimu kuwahusu.

“Kwa sasa, wazazi wengi wameteta kuhusu mihadarati, pombe haramu na mitambo ya Kamari. Kwenye tumepata habari kuhusu ukora wowote, kwa kawaida tumewajibikia kwa chini ya kipindi cha masaa 12. Ni vyema wananchi wahamasishwe kuwa wao ni washirika wetu wa dhati na wakitupasha habari, tunawajibika,” akasema.

Alikanusha habari kwamba maafisa wake wanaegemea mrengo wowote wa kisiasa akisema kuwa “sisi mirengo yote ni ya Wakenya na jukumu letu ni kulinda mioyo na mali bila ubaguzi kwa msingi wowote.”

[email protected]