MBALI na kuwa mfugaji hodari wa mbwa wa ulinzi eneo la Kabete, Kaunti ya Kiambu, Oscar Ragui pia ana mradi wa nguruwe.
Hata ingawa ni wanyama wa familia tofauti, Ragui anakiri mapato yao kifedha ni ya kuridhisha. Aliingilia ufugaji wa nguruwe miaka 15 iliyopita.
“Baba alikuwa na vizimba vya nguruwe ambavyo vilisalia wazi, akanishawishi nianze kuwafuga,” adokeza.
Aidha, alitumia mwanya wa jirani ambaye alikuwa akiuza nguruwe wanne.
Walikuwa watoto, na aliuziwa Sh2,500 kila mmoja, watatu wakiwa wa kike na mmoja kiume.
Chini ya kipindi cha muda wa mwaka mmoja, Ragui akawa mmiliki wa zaidi ya nguruwe 15.
Wanyama hao wanaofugwa nyumbani kwa minajili ya nyama na utengenezaji wa soseji, huzaa miezi mitatu majuma matatu na siku tatu baada ya kujamiishwa.
“Nguruwe wa miezi sita anapolishwa vizuri huwa tayari kujamiishwa,” Ragui anasema.
Kufikia mwaka wa 2010, mfugaji huyu anafichua alikuwa na zaidi ya nguruwe 100. Ana makazi yanayoweza kusitiri zaidi ya nguruwe 100. Kwa sasa, ana idadi jumla ya 15, wana wakiwa sita.
Mradi wa Ragui anauendeleza kwa minajili ya wale wa nyama – waliokomaa.
Anasema, kwa uchache ana wateja wafugaji wanaonunua wana. Akilinganisha bei ya nguruwe alipoingilia ufugaji na sasa, anasema kuna tofauti kubwa, kwa kile anataja kama “mabroka kuvamia soko”.
“Nguruwe wana wafugaji wengi, na mabroka wametumia mahangaiko yao kutafuta soko kuwakandamiza na kuwapunja,” Ragui anaelezea.
Anaongeza: “Kwa sababu wemapata mianya ya wachinjaji (akimaanisha wateja), baadhi yao wanaunda faida zaidi ya asilimia 100, mfugaji akiendelea kuumia.
Bei ya chakula cha mifugo, hasa cha madukani haikamatiki. Huku gharana ya malisho ikiendelea kuongezeka mara dufu, na ile ya nguruwe ikisalia ilipokuwa, Ragui anasema apu ya Bobbi aliyoianzisha 2019 inamsaidia kwa kiwango kikubwa kuondoa vikwazo vya soko.
“Kando na kunifaa kama mwasisi, imekuwa ya manufaa makubwa kwa wafugaji kijumla – waliojisajili,” asema.
Ina zaidi ya memba 1,000, wengi wao wakiwa wafugaji, wauzaji bidhaa za mifugo na mavetinari.
Programu hiyo ya kidijitali, unapojisajili na kuidhinishwa kuwa mwanachama (bila malipo), unapata fursa ya kipekee kupakia na kuchapisha picha za unachouza, zikiambatana na maelezo ulipo, bei na ikiwa kuna nafasi ya kupunguza bei.
“Hukagua kwa kina maombi ya machapisho, kabla kuyapakia mtandaoni,” Ragui ambaye ni adimini asisitiza, akidokeza kwamba apu hiyo inaendelea kuwafaa wafugaji na mavetinari.
Oscar Ragui, mfugaji wa nguruwe Kaunti ya Kiambu hutumia apu ya Bobbi kutafuta soko. PICHA | SAMMY WAWERU
“Baada ya kuizindua, nimeona bei ya nguruwe ikiimarika kwa sababu mabroka wamewekwa pembeni.”
Kwa sasa, huuza kivimbi mwenye umri wa miezi mitatu kuanzia Sh3,500. Waliokomaa, huuzia kichinjio cha Ndumbuini, kilichoko eneo la Kabete, Kiambu. Bucha hiyo ni maarufu katika uchinjaji na usambazaji wa nyama za nguruwe Kiambu na Kaunti ya Nairobi.
Ragui anasema kilo moja huuza kati ya Sh150 – 200.Kando na wafugaji, mavetinari waliojisajili wanaendelea kuridhia Bobbi.
“Kama mhudumu wa mifugo, apu hiyo imenifaa kwa kiwango kikuu. Ndiyo afisi yangu,” asema Mbugua Muthua, vetinari anayehudumu Kaunti ya Kiambu na Nairobi.
Apu hiyo inaendelea kujivunia umaarufu Kenya, Uganda na Tanzania.
Aidha, Ragui ameipa utambulisho wa Bobbi kutokana na ndege kipenzi chake aina ya Kasuku anayemuita Bobbi.
Ni nyuni anayefanya mazingira yake kusheheni ucheshi, kufuatia muigo wa mazungumzo.
Ragui anasema ni kwa muda tu ufugaji wa nguruwe umuingize katika ligi ya mamilionea nchini.