CHIPUKIZI wa Pelico Jam, ambayo ni timu ya Shule ya Upili ya Jamhuri, walitoka nyuma na kujibu magoli yake mawili dhidi ya FC Talents kusajili sare ya 2-2 katika mechi hiyo ya Ligi ya Kaunti ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Nairobi West, uwanjani Kihumbuini, Jumapili.
Katika mchuano huo uliopigwa kwa ustadi na kuibua msisimko wa hali ya juu, Pelico walitamba kipindi cha pili kwa kufuta magoli ya Talents kupitia Lawrence Migere katika dakika ya 51 na Jotham Wise kunako dakika ya 75.
Wapinzani wao walikuwa wamepata mabao kupitia kwa Brian Mbera katika dakika ya nne naye Nelson Ashira akiongeza la pili katika dakika ya 19.
Baada ya mechi kocha wa Pelico Jam Fred Amollo alikuwa na furaha tele.
“Mazoezi makali yalikuwa nguzo ya mchezo wetu,” alifichua kocha huyo.
Katika mechi nyinginezo za kiwango hicho, Red Carpet waliwinda Kuwinda United 2-0 katika Ligi ya Kanda, Nairobi West (NWRL), uga uo huo.
Carpet walifungua akaunti ya magoli kupitia Luiz Shanale dakika ya 60 Francis Mmani dakika ya 79.
Aidha, Ligi ya Kauntindogo (NWCL), Kibagare Spotiff waliwatandika Kangemi Atletico 2-1.
Kibagare Spotiff waliwatandika Kangemi Atletico 2-1. Picha/ Patrick Kilavuka
Sportiff walipata ushindi huo kupitia bao la kujifunga la Nelson Mandela dakika ya 14 na Hillary Kiplagat dakika ya 54. Atletico walifuta machozi dakika ya 47 kupitia Maxwell Mukundi.
Dreams iliwapepeta FC Talents Youth 4-3. Wafungaji wa Dreams walikuwa Oliver Mbugua kunako dakika ya 35 na Clift Mogire (3) dakika ya 45, 47 na 54 mtawalia. Youth waliyakomboa kupitia Elius Ongesa dakika ya 21 na Vincent Bukachi (2) dakika ya 33 na 42.