AJABU ya mmoja wa wanangu kunielekeza kwa kidole cha shahada, eti niende ghorofa ya pili na kujituliza huko ikiwa matumizi yake ya simu yananisinya, ni baadhi tu ya madhara ya maendeleo ya kiteknolojia anayokabiliana nayo mzazi wa leo.
Huo utachukuliwa kama utundu na wazazi wa kizazi changu na kilichokitangulia, lakini ndio uhalisia wa malezi ya siku hizi.
Eti mwanao ana shughuli mtandaoni, nawe vilevile una za kwako, hivyo nyinyi wateja sawa wa mtandao mnapaswa kubuni mazingira rafiki ili nyote wawili muufaidi.
Hivi nyumba hii ni ya nani? Mzazi anaweza kuuliza. Jawabu sahihi ni kwamba nyumba ni mzazi, ambaye pia ana jukumu la kumlisha, kumvisha na kumsitiri mwanawe.
Mzazi Mwafrika atakuja juu na kusema haya hayawezekani kwake, ni kinyume na desturi zetu, na kwamba akiyalazimishiwa atahama mtu, apende asipende.
Samahani mzazi mwenzangu. Huko kwa kauli yako kuwa sheria tumehama, wakubwa kwa wadogo wakajua haki zao, zikaimarishwa na sheria, suluhu ikawa majadiliano.
Bila shaka mzazi ana usemi kuhusu mambo mengi tu yanayofanyika nyumbani kwake, kuwe uzunguni au Afrika, lakini mataifa mengi yana sheria zinazomlinda mtoto kwa kumpa haki nyingi mno.
Nao utandawazi, ambao umewezeshwa na maendeleo ya kiteknolojia, dunia ikawa kijiji kimoja, umekuja na madhara yake.
Kuanzia vibonzo wanavyotazama kwenye runinga na mtandaoni hadi visa vya wazazi kuadhibiwa kisheria wakiwanyanyasa watoto wao, mambo yamewekwa mtandaoni na mtoto atayafikia popote alipo.
Anahitaji simu tu na muda wa kuvinjari mtandaoni, ghafla uhusiano kati yake nawe uanze kubadilika! Amejanjaruka. Anajua umebanwa na sheria. Utamwambia nini?
Lakini kwa sababu umekataa kutembea na majira, bado umekwama huko tulikotoka kwa mzazi kunguruma kama simba na kila kiumbe nyikani kunywea, utapata taabu sana.
Waweza kuwana kwa jino na ukucha kumweka mahali pake, lakini kumbuka hata akishindwa kukukabili kisheria anajua njia mbadala, ila potovu, za kumaliza ubishi haraka.
Kule mtandaoni amesoma hata njia za kujikatizia maisha akihisi hayana tija, hivyo usidhani una ukiritimba wa kumwamulia kila kitu.
Atajidhuru na kukusononesha milele. Haikosi umesoma matukio nchini Kenya ambapo watoto wametazama video fulani zinawakoroga akili na kuwafunza jinsi za kuangamiza jamaa zao na kuficha ushahidi.
Na labda uliwahi kumtukana somo wangu, Dkt Ezekiel Mutua, zama akidhibiti vya kutazamwa na kusikiwa alipokuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Halmashauri ya Kenya ya Uainishaji wa Filamu (KFCB).
Jichungue kisha utubu dhambi zako.
Zamani zetu tukikulia vijijini ilikuwa nadra kusikia fulani amejitia kitanzi, lakini leo hazipiti siku mbili bila habari za kuhuzunisha za aina hii.
Tukio kuu la hivi majuzi zaidi ni la mwanawe Mbunge Maalum, Bw David Sonkok, kujiua kwa kujipiga risasi kichwani, kisa na maana hakutaka kwenda shule.
Zamani zetu haikuwa hiari yako kusoma; kwenda shuleni kulikuwa miongoni mwa kanuni za familia zisizokiukwa kwa vyovyote vile, na aliyethubutu alihitajika kutafuta kwa kwenda! Lakini malezi yamebadilika siku hizi.
Unajipata ukimrai mwanao kufanya baadhi ya mambo, japo shingo upande, kwa sababu hutaki ukali wako umharibie maisha.
Nia ya mzazi kumlea mwana ni kumkuza hadi awe mtu mzima wa kujitegemea, si kumdhalilisha na kumkumbusha mkuu wake nyumbani ni nani. Anajua.
Mbinu yoyote ya malezi isiyomjenga mwana akawa raia mwema haifai kamwe. Ukimkalia mguu wa kausha atakuwa sugu.
Mabadilko ya mbinu za malezi, hasa kwa kuwa yametokea ghafla, yanaweza kuwawia ugumu wazazi, lakini hawana budi kuyakubali yalivyo. Ni nafuu kuliko kumponza mwana.