KAULI YA MATUNDURA: Waandishi watatu wa Zanzibar ‘wanaowakanganya’ wasomaji
NA BITUGI MATUNDURA
JUMA lililopita, wataalamu na wapenzi wa Kiswahili kutoka pembe mbalimbali za ulimwengu walifanya webina kumuenzi mwandishi na msomi Prof Said Ahmed Mohamed Khamis wa Zanzibar.
Kongandao hilo la Jumamosi, Aprili 30, 2022, liliandaliwa kwa ushirikiano wa Chama cha Waandishi wa Kiswahili (CHAWAKI), Chama cha Ukuzaji Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) na Nadj Media Center.
Webina hiyo ilielekezwa na Prof Leonard Muaka (Howard University), Prof Iribe Mwangi (Mwenyekiti, Chawaki) na Bw Hezekiel Gikambi. Wazungumzaji wakuu walikuwa Maprofesa Kimani Njogu na Aldin Mutembei.
Prof Said ni mmoja wa watunzi maarufu wa kazi za fasihi ya Kiswahili kutoka Zanzibar.
Waandishi wengine ni Mohamed Suleiman Mohamed (Nyota ya Rehema, Kiu na Kicheko cha Ushindi) na Muhammed Said Abdulla – aliyeandika riwaya za kiupelelezi k.m. Kisima cha Giningi – kwa kuathiriwa na Arthur Conan Doyle (Scotland), aliyeandika kazi zenye mhusika wa kiupelelezi, Sherlock Holmes anayelandana na Msa.
Mtaalamu mmoja kwenye webina ‘alishindwa’ kuwatofautisha Said Ahmed Mohamed (tuliyemuenzi) na Mohamed Suleiman Mohamed.
Majina ya watunzi hawa aghalabu huwakanganya wengi kwa sababu huendelezwa ifuatavyo katika tungo zao: S.A.Mohamed, Mohamed S. Mohamed na Muhammed Said Abdulla (Msa).
Wataalamu waliomuenzi Prof Said ni pamoja na: ‘MwanaNobel’ Abdulrazak Gurnah, mshairi Abdilatif Abdalla, Maprof Kithaka wa Mberia, Fikeni Senkoro, Obuchi Moseti, Farouk Topan, Inyani Simala, Robert Oduori, K.W.Wamitila, Pendo Malangwa, Mosol Kandagor, Clarissa Vierke na Ridha Samson (Japan). Wengine ni Dkt Keiko Takemura, Dkt Serena Talento miongoni mwa wengine.
Next article
Rais Kenyatta awasilisha bungeni majina ya watu 22…