MAKALA MAALUM: Wakazi wa Turkana kupata maji kaunti ikishirikiana na mashirika
NA SAMMY LUTTA
WAKAZI wa kijiji cha Nakorimunyen, Kaunti ndogo ya Loima, Turkana katika mpaka wa Kenya na Uganda sasa wanafurahia kuyapata maji bila kusafiri kilomita kadhaa kama zamani kutokana na kutekelezwa kwa miradi mingi ya uchimbaji visima.
Miradi hiyo imekuwa ikifanikiwa kutokana na mkataba wa ushirikiano ulioafikiwa kati ya serikali ya Kaunti ya Turkana pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali ya Oxfam na Epicenter Africa.
Kupitia maelewano hayo, mashirika hayo yanalenga kuvichimba visima 60 katika maeneo ya mashambani kisha kukarabati vile viliharibika. Mpango huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 15 ijayo na mashirika hayo mawili.
Taifa Leo ilipozuru kijiji hicho, ilikutana na Joyce Lonyaman, 12 ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi ya Namotuputh akifua nguo zake karibu na tangi kubwa la maji, wakati huu ambapo shule zimefungwa.
Tangi hilo ambalo maji yake huelekezwa ndani kupitia mabomba ya maji kwa kutumia kawi ya sola, ni kati ya yale yaliyojengwa na shirika la Oxfam na limekuwa likiwasaidia sana wakazi wa eneo hilo kwa miaka mingi.
Kando ya mahali anafulia nguo kuna kundi la ngamia ambao wanakula nyasi karibu na kanali ambapo maji kutoka mifereji ya tangi huelekezwa.
Kutokana na uwepo wa maji hayo eneo hilo limegeuka kisiwa kijani kibichi na mara nyingi hutumika kama malisho kwa ngamia.
Kwa mujibu wa Bi Lomyamana, mara nyingi wanapata maji mengi wakati ambapo kuna jua kwa sababu ya matumizi ya kawi ya sola ambayo pia inatumia miale ya jua.
“Mara nyingi hatuyapati maji kama hakuna jua kwa sababu maji hungia kwenye tangi kupitia presha ya kawi ya sola,” akasema.
Anasifia kuwa uwepo wa tangi hilo umewasaidia sana kwa kuwa hapo zamani wafugaji waliokuwa na mifugo wengi, walikuwa wakielekea hadi nchi jirani ya Uganda, kusaka maji au katika kijiji jirani cha Namoruputh.
Kwa mujibu wa Naibu Gavana wa Turkana Peter Lotethiro, mkataba kati ya kaunti na shirika la Oxfam, unalenga kuhakikisha kuwa maelfu ya wakazi wanaokabiliwa na janga la njaa pia wanasaidiwa kwa kupewa maji safi na vyakula.
Bw Lotethiro alisema kuwa kupitia makubaliano hayo, visima vya maji ambavyo viliharibika pia vitakarabatiwa ili kuwazuia wenyeji kutembea kilomita kadhaa kusaka maji.
“Visima hivyo 60 vipo katika kaunti ndogo zote tano ambazo ni Loima, Turkana ya Kati, Turkana Mashariki, Turkana Kusini na Turkana Kaskazini. Huu ni mwanzo tu na kutokana na ufanisi wa mradi huo, tutaueneza hadi maeneo mengine hadi kila mwananchi hapa Turkana aweze kupata maji safi kwa matumizi nyumbani na kunywa,” akasema.
Afisa Mkuu wa Maji wa kaunti Moses Natome alisema kuwa ripoti ya ukaguzi wa visima 1,800 kote katika kaunti hiyo, umeonyesha kuwa asilimia 40 ya visima vyote vilivyochimbwa mashinani havifanyi kazi baada ya kutelekezwa.
Naye Bi Irene Gai ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usambazaji maji kutoka shirika la Oxfam tawi la Kenya, alisema lengo lao kuu ni kushirikiana na serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa wakazi wa Turkana wanapata bidhaa hiyo na kumaliza matatizo ya tangu kale ambapo wafugaji wa kuhamahama hulazimika kuingia hata nchi jirani ya Uganda kusaka maji.
Bi Gai alisema kuwa ni jambo la kufurahisha kuwa kampuni katika sekta ya kibinafsi zimeanza kuwekeza katika sekta ya uchimbaji visima kama njia ya kuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo kame kama Turkana, hawateseki kutokana na ukosefu wa maji.
Naye Afisa Mkuu Mtendaji wa Epicenter Afrika, Mary Njue alisema kuwa shirika hilo limekuwa likiendeleza miradi ya maji katika maeneo kame ikiwemo Turkana kwa muda wa miaka 10 iliyopita na akaahidi kuwa watahakikisha kuwa miradi yote inakamilishwa jinsi walivyoagana na utawala wa kaunti.
Waziri wa Maji katika Kaunti ya Turkana Vincent Palor alisikitika kuwa ukame unaendelea kuwaathiri wakazi hasa katika maeneo kama ila akasema kuwa utawala wa gatuzi hilo umepiga hatua kubwa katika kuwekeza kwenye miradi ya maji.
Waziri wa Maji katika Kaunti ya Turkana Vincent Palor akihutubia wanahabari. PICHA | SAMMY LUTTA
“Tumebaini kuwa uchimbaji wa visima ndio njia faafu zaidi ya kuhakikisha kuwa wakazi wa Turkana wanapata maji safi ya shughuli zao za nyumbani na pia kunywa. Changamoto hata hivyo ni ukosefu wa fedha kwa sababu kiwango cha bajeti kinachotengewa idara hiyo huwa ni chini mno,” akasema Bw Palor.
“Kama kaunti, tunahitaji kutengewa Sh2.5 bilioni kila mwaka ila tumekuwa tukitengewa Sh300 milioni. Iwapo tutatengewa fedha zaidi, basi miradi mingi iliyoanzishwa ya uchimbaji visima itakamilishwa na kutekelezwa kwa wakati,” akaongeza.
Mnamo Jumanne, ulimwengu uliadhimisha Siku ya Maji Duniani wakati ambapo maeneo mengi nchini yanakubwa na ukame pamoja na njaa.
Bw Parlor alisema wakati wa maadhimisho hayo kuwa serikali kuu inafaa kushirikiana na kaunti kuhakikisha miradi mingi ya maji inakumbatiwa hasa mashinani badala ya kumakinikia mijini pekee.
Hasa alitaja kilimo cha unyunyuziaji wa mashamba maji kama mradi ambao utasaidia sana wakazi wa maeneo kame kujitegema au kujitosheleza kupitia uzalishaji wa vyakula.