Jinsi Kibaki alivyokaidi Kenyatta mara 2
NA STEPHEN MUNYIRI
WAKENYA wanapoendelea kumwomboleza Rais Mstaafu Mwai Kibaki, ambaye atazikwa nyumbani kwake Othaya katika Kaunti ya Nyeri, Jumamosi, Aprili 30, 2022 atakumbukwa kwa ushujaa wake na jinsi alivyowathamini marafiki na kusisitiza haki kwa wote.
Mnamo Machi 1975, Kibaki wakati huo akiwa waziri katika utawala wa Mzee Jomo Kenyatta, alimkaidi rais na kuhudhuria mazishi ya Josiah Mwangi Kariuki maarufu kama JM Kariuki.
Serikali ya Mzee Kenyatta ilikashifiwa na hata kuhusishwa na kifo cha JM, ambaye alikuwa mbunge wa Nyandarua Kaskazini (saa eneobunge la Kinangop) kutokana na jinsi alivyoikosoa hasa kuhusu masuala ya ardhi.
Bw Mwangi aliibua semi maarufu kuwa kutokana na ulafi wa viongozi serikalini waliokuwa wakitwaa na kupora mali ya umma baada ya uhuru, Kenya ingesalia taifa la watu 10 ambao ni mamilionea huku watu milioni 10 wengine wakiishi katika umaskini mkubwa.
Katika mahojiano na Taifa Leo, mshirika wa karibu wa Mzee Kibaki, Joe Wanjau, ambaye alikuwa kiongozi wa wanafunzi mnamo 1975 katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema kuwa Kibaki alikuwa na ujasiri na kukaidi agizo la Mzee Kenyatta kwa mawaziri wake wasihudhurie mazishi hayo.
Bw Wanjau, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kutoka Nyeri, anasema walihofia hatua ya Kibaki kuhudhuria mazishi hayo kungesababisha atimuliwe kazini na Mzee Kenyatta.
“JM alipofariki kwa njia tata kulikuwa na fujo na wanafunzi wa vyuo vikuu waliamua kuwa lazima tuhudhurie mazishi yake. Tulishangaa kuwa mawaziri wengine walisusia mazishi hayo isipokuwa Kibaki,” akasema Bw Wanjau.
Alikumbuka kuwa rambirambi ya serikali ilisomwa na marehemu Simeon Nyachae ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kati enzi hizo.
“Waombolezaji walikataa rambirambi ya serikali na kumzomea Nyachae. Kibaki pekee ndiye mtu wa upande wa serikali aliyeruhusiwa kuzungumza,” akasema Bw Wanjau.
Akihutubu wakati wa mazishi hayo, Kibaki, ambaye alikuwa anaonekana amekasirika, aliahidi kuwa lazima kifo cha JM kingechunguzwa hata kama ingechukua muda wa zaidi ya miaka 100 ili kupata ukweli.
Hadi sasa kiini cha mauaji ya JM hakijawekwa wazi.JM Kariuki aliuawa Machi 2, 1975, ambapo maafisa wa serikali waliokuwa karibu na Kenyatta walishukiwa kuhusika.
Mwili wake ulipatikana msituni Ngong na mchungaji ng’ombe.
Baada ya mauaji ya JM Kariuki, Kibaki aliwekewa shinikizo kutangaza uaminifu wake kwa Mzee Kenyatta hasa baada yake kuhudhuria mazishi kinyume na agizo la Mzee Kenyatta.
Awali mnamo 1969, Kibaki na JM ndio wanasiasa pekee wa ngazi za juu kutoka eneo la Mlima Kenya ambao walihudhuria mazishi ya Tom Mboya katika Kisiwa cha Rusinga.
Mauaji ya Mboya yalikuwa yamesababisha uadui mkubwa kati ya Wakikuyu na Wajaluo.
Wakereketwa wa Mzee Kenyatta pia walikuwa wamelaumiwa kuhusiana na mauaji ya Mboya, ambaye nyota yake ya kisiasa ilikuwa ikiendelea kung’aa kote nchini.
Katika maisha yake ya kisiasa, Kibaki alichukua msimamo wa kitaifa akiepuka kuonekana kama kiongozi wa kikabila, ndiposa alikuwa akikataa kujihusisha na muungano wanasiasa wa makabila ya Gikuyu, Embu na Meru (GEMA), ambao ulianzishwa mnamo 1971 ukiongozwa na Mzee Kenyatta, Gikonyo Kiano na Jeremiah Nyaga.
Mnamo 1973 katika mkutano uliofanyika Nyeri na Njenga Karume akachaguliwa kiongozi wake, Kibaki aliendelea kukataa kujihusisha na kundi hilo.