Kioja hakimu akifanyia washtakiwa wa wizi harambee kortini
NA BRIAN OCHARO
GHARAMA ya juu ya mahitaji ya kimsingi inawasukuma Wakenya wengi kutumia njia zisizo za kawaida za kujikimu ili kuepuka kulala njaa.
Wanandoa huko Mombasa ni kati ya Wakenya waliobanwa sana na maisha hadi wakaamua kuiba kilo moja ya unga ili kuwazuia watoto wao kulala njaa.
Lakini hawakubahatika kwani walikamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu shtaka hilo.
Saumu Ali na mumewe Evans Odhiambo, walifikishwa mbele ya Hakimu Vincent Adet.
Hati ya mashtaka ilisema washukiwa hao waliiba kilo moja ya unga wa ngano mnamo Aprili 13, katika eneo la Shimanzi, Kaunti Ndogo ya Mvita.
Wawili hao walikiri shtaka hilo lakini wakasema walikuwa wamekosa namna na wakaonelea lilikuwa jambo la busara kufanya siku hiyo ili kuepuka kulala njaa.
“Nilikuwa nikifanya kazi yangu ya vibarua wakati Bw Odhiambo aliponiita ili nimsaidie kubeba mizigo. Tulifanya hivi kwa ajili ya watoto wetu,” mwanamke huyo alisema.
Mwanamke huyo aliambia mahakama kwamba alikiri kwa afisa aliyemkamata na kueleza hali yake lakini afisa huyo alisisitiza kumpeleka mahakamani.
“Tulichukua unga huo kutoka kwa gari lililokuwa limeegeshwa karibu na barabara. Bw Odhiambo aliniomba nimsaidie kubeba mizigo hiyo,” aliambia mahakama.
Bw Adet hata hivyo, aliamua kuchukua njia tofauti kuwasaidia.
“Kwa misingi ya kibinadamu, hasa kwa mwanamke huyu, nimezingatia mazingira ya kosa hilo na ninamhurumia kwa hali yake. Kuwa na watoto watatu bila mapato ni jambo ngumu, nina maoni kwamba tumnunulie unga na nyama kwa leo,” alisema Adet.
Na kutokana na hili, hakimu aligeuza kikao cha mahakama kuwa harambee na kuanza kwa kutoa mchango wake wa Sh1,000.
Kisha akawataka wote waliokuwepo mahakamani wakati huo kuchangia chochote cha kuongeza ili kuwanunulia wawili hao nyama na unga.
Mwishoni mwa mchango huo, hakimu alimwambia mwanamke huyo kwamba amesamehewa kwa kosa lake na kuwaachilia huru, lakini akawashauri wasirudie kosa hilo.
Hakimu alieleza kuwa uamuzi wake ulitokana na ripoti ya uchunguzi wa tabia za washtakiwa, ambayo ilionyesha kwamba wawili hao hawakuwa na njia ya kujiletea mapato na walikuwa wakitegemea kazi duni.
Next article
Sonko, Nassir kukutana ana kwa ana hafla ya Azimio Tononoka