‘Muthama hataki kuwa katika jukwaa moja na Alfred Mutua’
NA JUSTUS OCHIENG
HATUA ya kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap Dkt Alfred Mutua kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza wake Naibu Rais William Ruto inaendelea kusababisha joto baada ya Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnson Muthama kuipinga.
Bw Muthama alisema hawezi kufanya kazi na Gavana huyo wa Machakos kutokana na kile alichotaja kama “maovu” ambayo Dkt Mutua amefanya katika kaunti hiyo.
Seneta huyo wa zamani wa kaunti hiyo Jumatano, Mei 11, 2022 alisema hiyo ndio maana alikosa kuhudhuria mkutano wa kisiasa wa kumkaribisha Dkt Mutua ndani ya Kenya Kwanya, licha ya kufanyika karibu na nyumbani kwake eneo la Tala Jumanne, Mei 10, 2022.
Mkutano huo wa kampeni uliongozwa na Dkt Ruto na kuhudhuriwa na vinara wengine wa muungano huo kama vile kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, mwenza wa Ford Kenya Moses Wetang’ula, miongoni mwa viongozi wengi.
“Sikuhudhuria mkutano huo wa kisiasa kutokana na sababu zangu. Ni wazi kwamba nimepambana na Mutua kwa miaka tisa na miezi tisa,” Muthama akaambia Taifa Leo kwenye mahojiano kwa njia ya simu.
“Ikiwa hivyo ndivyo watu huniona na kunijua, sababu gani nitatoa nikiamka siku moja asubuhi na watu wakaniona nikisaka densi na Mutua nikisema kuwa nitafanyakazi naye kuanzia sasa kuendelea mbele?”, Bw Muthama akauliza.
“Ikiwa ni lazima nionekane hadharani na Mutua, sharti kwanza niketi naye na nimwambie hivi: ‘Waonyeshe watu wa Machakos maji ya mifereji ambayo ulisema umeweka katika kila boma, nionyesha vifaranga uliosema ulisambaza kwa kila familia na ambulansi ambazo ulinunua’” Bw Muthama akasema.
Vile vile, alihoji yaliko matrakta ambayo yalinunuliwa na utawala wa Dkt Mutua.
Bw Muthama alisema japo Dkt Mutua yu huru kujiunga na UDA n ahata kumuunga mkono Dkt Ruto, lazima awajibike kwa watu wa kaunti ya Machakos.
“Hiyo ndio inanifanya kuwa tofauti na wanasiasa wengine. Mimi ni mwenyekiti wa UDA lakini sharti nizingatie misimamo, maadili na imani yangu,” akasema.
Tulipomfikia kwa njia ya simu, Dkt Mutua akidinda kujibu madai ambayo yaliyotolewa na Bw Muthama.
Mnamo Jumatatu alipuuzilia mbali madai ya Katibu Mkuu wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Junet Mohamed kwamba aliitisha fedha ili aendelee kusalia ndani ya muungano huo.
Bw Mohamed ambaye pia ni Mbunge wa Suna Mashariki alidai kuwa wale walioondoka Azimio walitaka msamaha kutoka kwa Bw Odinga kuhusiana na kesi za ufisadi zinazowazonga.
Hata hivyo, Dkt Mutua alipuuzilia mbali madai hayo akisema ni ya uwongo.
“Ni uwongo. Wananipiga vita kwa sababu ya msimamo wangu. Sawa na mpango wao wa kututenga, watafeli,” akasema.