Ukraine yaeleza kupata miili 410
NA AFP
KYIV, UKRAINE
UKRAINE imesema imepata miili 410 ya raia wake wanaoaminika kuuawa na vikosi vya Urusi kwenye maeneo iliyotwaa kutoka udhibiti wa vikosi hivyo.
Taarifa hizo zilitolewa Jumatatu na Kiongozi Mkuu wa Mashtaka nchini humo, Iryna Veneditova.
“Miili 410 ya raia ilitolewa kwenye maeneo tuliyotwaa kutoka kwa vikosi vya Urusi, karibu na mji mkuu, Kyiv. Wachunguzi tayari wameikagua miili 140,” akasema, kwenye mahojiano na kituo rasmi cha televisheni cha serikali.
Ukraine ilitwaa maeneo hayo kutoka kwa Urusi wikendi iliyopita.
Taifa hilo limeilaumu Urusi kwa kuendesha “mauaji ya halaiki” katika mji wa Bucha, ulio umbali wa kilomita 30, kaskazini mashariki mwa Kyiv.
Jumapili, meya wa Bucha, Anatoly Fedoruk, aliliambia shirika la AFP kwamba miili 280 ilizikwa katika makaburi ya pamoja.
Miili ya raia pia ilipatikana kwenye barabara za mji huo, huku vikosi vya Ukraine vikiendelea kutwaa maeneo yake muhimu.
Jumapili, wanahabari wa AFP walihesabu miili 20 kwenye barabara moja pekee mjini humo. Mmoja wa waathiriwa alikuwa amefungwa kamba mikononi mwake, ijapokuwa waathiriwa wote walikuwa wamevalia mavazi ya kiraia.
Viongozi wa eneo hilo waliwaonyesha wanahabari hao kaburi la pamoja Jumapili. Walisema kuwa watu 57 walizikwa katika moja ya makaburi hayo. Vile vile, walieleza kuwa uchunguzi wao umebaini kwamba baadhi ya miili haijazikwa vizuri.
Urusi
Licha ya hayo, Urusi imekuwa ikikanusha kuhusika kwenye mauaji hayo.
Badala yake, imekuwa ikitaja madai hayo kama “propaganda zinazoendeshwa na Ukraine na vyombo vya habari vya mataifa ya Magharibi.”
“Wakati ambapo vikosi vyetu vilikuwa vikiudhibiti mji huo, hakuna raia hata mmoja aliyekumbana na mashambulio yoyote,” akasema waziri wa Ulinzi wa Urusi.
Urusi ilichukua udhibiti wa Bucha siku tatu pekee baada ya kuanza uvamizi wake dhidi ya Ukraine, Februari 24.
Kando na Bucha, Ukraine pia inailaumu Urusi kwa kuendesha uhalifu katika mji jirani wa Irpin, ambapo kama Bucha, miundomsingi yake mingi imeharibiwa kabisa.
Maafisa wa serikali ya Ukraine wanasema kuwa karibu watu 200 waliuawa katika mji huo, ambao pia ulitekwa na Urusi siku za mwanzo za uvamizi huo.
Wakati huo huo, Rais Volodymyr Zelensky jana Jumatatu aliilaumu Urusi kwa kuendesha mauaji ya kimbali katika nchi yake.
Jana Jumatatu, viongozi kadhaa wa nchi za Magharibi waliikashifu vikali Urusi kwa ukatili wake, baada ya picha kadhaa kusambazwa mitandaoni zikionyesha kiwango kikubwa cha uharibifu kwenye miji iliyoachwa na vikosi hivyo.
“Haya ni mauaji ya kimbari. Vitendo hivi ni sawa na kuwaodoa raia katika taifa lao,” akasema Rais Zelensky, kwenye mahojiano na kiuo cha televisheni cha CBS.
“Sisi ni raia wa Ukraine na hatutaki kuanza kutawaliwa kwa misingi ya sera na mwongozo wa Urusi. Hiyo ndiyo sababu tunaangazimwa kwa njia zote,” akasema.
Umoja wa Mataifa (UN) nao ulisema kuwa kupatikana kwa makaburi ya halaiki mjini Bucha kumeibua maswali kuhusu ukatili uliofanywa na wanajeshi wa Urusi.
Ulisema kuna haja ya wale waliothiriwa kuhifadhi ushahidi wa vitendo hivyo.
“Matukio haya yanaibua maswali mengi kuhusu uwezekano mkubwa wa Urusi kukiuka sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu,” ikaeleza afisi ya UN kuhusu haki za binadamu.